Miradi inayoendelea
MIRADI INAYOENDELEA
Mapitio ya Sheria ya Bima za Magari, Sura ya 169
Sheria ya Bima za Magari, Sura ya 169 ni mojawapo ya Sheria kongwe nchini. Sheria hii ilitungwa mwaka 1945 na kuanza kutumika mwaka 1946, ikiwa na lengo la kuweka masharti ya bima dhidi ya majanga kwa mtu wa tatu (third party) yanayotokana na matumizi ya magari.
Kwa muda mrefu, Sheria hii imeendelea kutumika bila kufanyiwa maboresho, jambo lililosababisha changamoto katika utekelezaji wake kutokana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kiteknolojia na kimazingira.
Lengo la mapitio haya ni kubainisha changamoto za kisheria katika utekelezaji wa Sheria ya Bima za Magari ili kupendekeza maboresho yatakayosaidia kupunguza changamoto katika upatikanaji wa fidia kwa waathirika wa ajari za barabarani.
2. Mapitio ya Sheria ya Bima, Sura ya 394
Sheria ya Bima, Sura ya 394 ilitungwa mwaka 2009 na kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania kwa ajili ya kuratibu na kusimamia biashara ya bima nchini. Tangu kutungwa kwa Sheria ya Bima kumekuwa na mabadiliko katika usimamizi wa sekta ya bima kutokana na kasi ya ukuaji wa sekta ya bima pamoja na maendeleo ya teknolojia na uvumbuzi hivyo Sheria kutokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Mapitio ya Sheria ya Bima, Sura ya 394 yanalenga kubainisha changamoto za kisheria katika usimamizi wa sekta ya bima ili kupendekeza maboresho ya kuweka mazingira wezeshi ya kisheria kwa manufaa ya wadau wote, sambamba na kulinda maslahi ya wananchi na maendeleo ya sekta ya fedha nchini.
3. Mapitio ya Sheria ya Afya na Usalama Mahala pa Kazi, Sura ya 297
Sheria hii ni moja ya sheria zinazohusika kwa namna moja au nyingine katika kusimamia na kuratibu shughuli za uwekezaji na biashara. Mapitio yanafanyika ili kubaini changamoto za kisheria zinazojitokeza katika utekelezaji wa sheria hiyo na kupendekeza marekebisho yatakayosaidia kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara.
4. Mapitio ya Sheria ya Usuluhishi, Sura 15
Tume inafanya Mapitio ya Sheria ya Usuluhisho kwa lengo la kubaini changamoto zilizopo katika utekelezaji wa sheria hiyo ili kutoa mapendekezo kwa serikali hatua stahikikwa kuhakikisha migogoro ya kibiashara inatatuliwa kwa haraka na kaurahisisha ufanyaji wa biashara.
5. Tathmini ya Utekelezaji wa Sheria za Mamlaka ya Nchi kuhusu Umiliki wa Utajiri Asili na Maliasili za Nchi, Sura ya 449 na Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti hasi katika Mikataba ya Utajiri Asili na Maliasili za Nchi, Sura ya 450.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga Sheria ya Mamlaka ya Nchi katika Umiliki wa Mali na Rasilimali Asilia, Sura 449 na Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Mali na Rasilimali Asilia, Sura ya 450 kwa lengo la kusimamia mali na rasilimali asilia. Sheria hizi pamoja na masuala mengine zinaweka misingi ya kuzingatiwa katika usimamizi wa mali na rasilimali asilia. Misingi hiyo ni: haki ya umiliki na udhibiti; kunufaika; uwazi na uwajibikaji; usawa; uendelevu; ushindani; na uzingatiaji wa sheria, kanuni na mikataba.
Lengo la mapitio haya ni kuangalia uzingatiwaji wa misingi iliyoainishwa katika sheria za usimamizi wa mali na rasilimali asilia za nchi katika sekta zinazoratibu uhifadhi, utafutaji, umiliki na uvunaji wa mali na rasilimali asilia za nchi. Tathmini itabainisha ufanisi na changamoto katika utekelezaji wa masharti yanyohusu uwekezaji katika mali na rasilimali asilia za nchini na kutoa mapendekezo ya kuboresha mfumo wa kisheria ili kuvutia uwekezaji na kuhakikisha ulinzi wa mali na rasilimali asilia ili kuwanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.
6. Tathmini ya Utekelezaji wa Sheria ya Ugaidi, Sura ya 19
Tathini inafanyika ili kuangalia ni kwa kiwango gani malengo ya kutungwa kwa sheria hiyo yamefikiwa na kubainisha changamoto zinazoathiri utekelezaji wa sheria ili kutoa mapendekezo ya namna ya kuboresha.