Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

SERIKALI YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA 2025/2026 YA LRCT- NAIBU WAZIRI.
14 May 2026
SERIKALI YARIDHISHWA...

Naibu waziri Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Zainabu Katimba amesema Serikali inaridhishwa na utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo imeendelea kufanya tafiti na mapitio ya sheria mbalimbali pamoja na kutoa elimu ya sheria kwa umma.

Kauli hiyo ameitoa tarehe 14/05/2026 katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama uliopo mjini Dodoma wakati wa kikao cha 24 cha Baraza la wafanyakazi wa Tume hiyo ambapo ameeleza kwamba Tume imefanya mapitio ya sheria muhimu zikiwemo Sheria ya Usuluhishi, Sura ya 15; Sheria ya Bima, Sura ya 394; na Sheria ya Bima za Vyombo vya Moto (Magari) Sura ya 169, kwa lengo la kuhakikisha zinaendana na mahitaji ya sasa ya kijamii na kiuchumi.

Mhe. Katimba alifafanua kwamba Tume inaendelea na mapitio ya Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi, Sura ya 295, Tathmini ya utekelezaji wa sheria zinazohusu umiliki wa mali na rasilimali asilia pamoja na kufanya tafiti katika maeneo mapya kama matumizi ya Akili Unde (Artificial Intelligence), biashara ya hewa ya ukaa, adhabu ya kifo na kifungo cha maisha, na usajili wa mawakili.

“Hatua hizi zinaonesha mchango mkubwa wa Tume katika kusaidia Serikali kuwa na sheria zinazoendana na mabadiliko ya teknolojia, uchumi na mahitaji ya wakati” alieleza Mhe. Katimba.

“Ninapenda kutambua kwa heshima kubwa juhudi zinazoendelea kufanywa na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania katika kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kuishauri Serikali kuhusu maboresho ya sheria mbalimbali kwa ajili ya kuendana na mahitaji ya wakati na maendeleo ya Taifa letu” Aliendelea Kusema.

Aidha Katika mwaka wa fedha 2025/2026, Tume imewasilisha taarifa tano (5) kwa waziri wa katiba na Sheria ambazo ni Taarifa ya Mapitio ya Sheria ya Takwimu, Sura ya 351 na Taarifa kuhusu Utafiti wa Mfumo wa Sheria Zinazosimamia Vyama vya Ushirika, za Februari,2025; Taarifa ya Mapitio ya Sheria Zinazosimamia Udhibiti wa Matumizi ya Bidhaa za Tumbaku, Shisha na Sigara za Kielektroniki, Taarifa ya Tathimini ya Utekelezaji wa Sheria ya Michezo ya Kubahatisha Nchini, Sura ya 41 na Taarifa ya Utafiti kuhusu Mfumo wa Sheria Zinazosimamia Utatuzi wa Migogoro ya Mikopo katika Benki na Taasisi za Fedha, zote za Julai, 2025.

Awali akimkaribisha Waziri huyo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bw. George Mandepo alisema Mkutano huo utakuwa na mada zitakazo wasilishwa kwa lengo kuongeza uelewa wa shughuli za Tume, kukuza ujuzi na uzoefu katika kuimarisha utendaji kazi ambazo ni Mada kuhusu ukamilishwaji wa Mpango Mkakati wa Tume wa miaka mitano 2026/2027 – 2030/2031; Mada kuhusu Elimu ya usimamizi wa Fedha (Financial Literacy); na Mada kuhusu Maana ya Maadili na Umuhimu wa Uadilifu katika Utumishi wa Umma.

Aidha Bw. Mandepo alieleza kuwa mwaka wa fedha 2025/2026, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania iliidhinishiwa na Bunge kutumia jumla ya Shilingi bilion 7.45 Kati ya fedha hizo, kiasi cha Shilingi bilion 1.775 ikiwa ni kwa ajili ya Mishahara na kiasi cha Shilingi bilion 5,627 ikiwa ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo.