Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

BALOZI LUVANDA AITAKA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA KUTATUA CHANGAMOTO ZA KISHERIA KABLA HAZIJAWA MALALAMIKO YA JAMII.
08 Aug 2026
BALOZI LUVANDA AITAK...

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Balozi Baraka Haran Luvanda ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kuangalia  changamoto za kisheria zilizopo katika jamii na kufanya maboresho kabla jamii haijaanza kuwa na malalamiko kuhusu changamoto hizo.

Balozi Luvanda, alitoa wito huo alipotembelea banda la Tume ya Kurekebisha Sheria tarehe 8 Agosti 2026 katika Maonesho ya kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nanenane) katika viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Jijini Dodoma.

Alieleza Tume inapaswa kuwa mbele kuwaza katika kutatua matatizo ya kisheria bila kusubiri jamii kujitokeza kutoa malalamiko badala yake malalamiko husika ya kisheria yaanze kubainika kupitia Utafiti  na yaweze kutatuliwa mapema.

"Mnatakiwa muwe pro active msisubiri mpaka wananchi walalamike ndio muingie kuanza kufanya mchakato wa maboresho ya sheria bali mnapaswa nyinyi muwe mbele yao, muanze kujua changamoto za kisheria kisha mzifanyie kazi kabla wananchi hawajalalamika kuhusu mapungufu hayo ya kisheria" alisema Balozi Luvanda.

Awali Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Tume ya Kurekenisha Sheria,  Bi.Vicky Mbunde, alieleza nafasi ya Tume hiyo katika kushiriki Maonesho ya Nanenane   kuwa ni kutoa elimu ya sheria kwa jamii, kupokea maoni na kuwaeleza kuhusu nafasi ya Tume katika maboresho ya Sheria ili kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
"Tumefanikiwa kuwaeleza wananchi kuhusu majukumu ya Tume ya Kurekebisha Sheria lakini pia tumepokea maoni ya maboresho ya sheria mbalimbali na sisi tunakwenda kuyafanyia kazi ili kuhakikisha sheria zilizopo zinaendana na wakati na mahitaji ya jamii kwa wakati wa sasa" Alisema Bi. Vicky

Aidha, akifafanua zaidi kuhusu umuhimu wa utafiti wa sheria Bi. Vicky alisema  Tume hiyo imekua ikifanya tafiti ikiwa kuna eneo jipya ambalo halina usimamizi wa kisheria lakini jamii ina matumizi nalo na kwamba baada ya kufanyika kwa utafiti hutolewa Taarifa ya mapendekezo kuhusu kutungwa kwa sheria mpya au kufanyika kwa maboresho ya Sheria zilizopo ili kuanisha takwa hilo jipya kwa watumiaji.

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeshiriki Maonesho ya  Kilimo, Mifugo na Uvuvi (Nanenane) Jijini Dodoma yaliyoanza tarehe 1/8/2026 hadi 8/8/2026 ili kutoa elimu ya sheria kwa wananchi na kupokea maoni na mapendekezo ya maboresho ya sheria mbalimbali.