Vijana nchini wamehimizwa kutumia mitandao ya kijamii kwa uwajibikaji na kuzingatia sheria za nchi, wakikumbushwa kuwa matumizi mabaya ya majukwaa hayo yanaweza kusababisha hatua za kisheria kwa kuwa sheria ina mkono mrefu.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Bi. Zainab Chanzi, wakati wa Maonesho ya Wakulima ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni, mkoani Dodoma.
Bi. Chanzi amesema kuwa ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano umeongeza fursa za kujifunza, kufanya biashara na kubadilishana taarifa, lakini pia umeambatana na changamoto zinazotokana na matumizi yasiyo sahihi ya mitandao ya kijamii.
Ameeleza kuwa baadhi ya watumiaji, hususan vijana, wamekuwa wakichapisha au kusambaza maudhui yanayokiuka sheria bila kutambua athari zake, jambo ambalo linaweza kuwafanya kuwajibika mbele ya vyombo vya sheria.
Ni muhimu kwa vijana kufahamu kuwa kila wanachochapisha au kusambaza kwenye mitandao ya kijamii kinaweza kuwa na madhara ya kisheria endapo kitakiuka sheria za nchi.
Sheria ina mkono mrefu, hivyo wanapaswa kutumia mitandao hiyo kwa busara na uwajibikaji," amesema Bi. Chanzi.
Ameongeza kuwa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inaendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kutoa elimu ya sheria kwa wananchi ili kuongeza uelewa kuhusu haki, wajibu na umuhimu wa kuzingatia sheria katika matumizi ya teknolojia na nyanja nyingine za maisha.
Aidha, amewahimiza wananchi kutembelea banda la tume hiyo katika maonesho hayo ili kupata elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria na kupata ufafanuzi kuhusu sheria zinazohusu matumizi ya mitandao ya kijamii na maendeleo ya teknolojia