Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

WANAFUNZI WA ZUZU SEKONDARI WAJIFUNZA MCHAKATO WA UBORESHAJI WA SHERIA - LRCT
04 Aug 2026
WANAFUNZI WA ZUZU SE...

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Zuzu ya mkoani Dodoma leo wametembelea banda la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, kwa lengo la kujifunza mchakato wa kutunga na kuboresha sheria nchini.

Katika ziara hiyo ya kielimu, wanafunzi hao walipata fursa ya kuzungumza na Mwanasheria Mwandamizi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Vicky Mbunde, ambaye aliwaeleza majukumu ya Tume pamoja na hatua mbalimbali zinazofuatwa katika kufanya mapitio, kuboresha na kupendekeza marekebisho ya sheria ili ziendane na mahitaji ya wakati na maendeleo ya jamii.

Akizungumza na wanafunzi hao, Mbunde aliwahimiza kujenga utamaduni wa kuifahamu sheria na kuheshimu utawala wa sheria, akieleza kuwa vijana ni wadau muhimu katika maendeleo ya taifa na wana nafasi ya kushiriki kutoa maoni yanapohitajika katika maboresho ya sheria.

Kwa upande wao, wanafunzi wa Zuzu Sekondari walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema imewaongezea uelewa kuhusu nafasi ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na mchakato unaotumika kutunga au kuboresha sheria nchini.

Maonesho ya Nane Nane yanaendelea kuvutia wanafunzi, wakulima na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini, yakitoa fursa ya kujifunza huduma na shughuli zinazotekelezwa na taasisi za umma na binafsi kupitia mabanda ya maonesho.