Watumishi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania wamemtunuku Tuzo maalum Katibu Mtendaji wa taasisi hiyo, Bw. George Mandepo, ya kutambua mchango wake mkubwa katika kuimarisha utendaji kazi, ushirikiano na maendeleo ya watumishi ndani ya Tume hiyo.
Tuzo hiyo ilitolewa na watumishi wakati wa Kikao cha Baraza la 24 la Wafanyakazi lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama uliopo mjini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi pamoja na wawakilishi wa watumishi wa taasisi hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya watumishi wa Tume hiyo wakati wa kikao hicho ,Mwenyekiti wa TUGHE tawi hilo Bi. Vicky Mbunde alisema Bw. Mandepo ameonyesha uongozi wenye weledi, uwajibikaji na usikivu kwa watumishi, hali iliyochangia kuongezeka kwa morali ya kazi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya watumishi wa Tume ya Kurekebisha Sheria.
“Katika kipindi cha uongozi wake, tumeshuhudia mazingira bora ya kazi, ushirikiano mzuri baina ya Menejimenti na Watumishi pamoja na kuongezeka kwa ari ya utendaji ndani ya Taasisi,” alisema Vicky Mbunde.
Watumishi hao walieleza kuwa tuzo hiyo ni ishara ya kuthamini juhudi za Katibu Mtendaji katika kusimamia kwa karibu utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania pamoja na kuhamasisha uwajibikaji kwa watumishi.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria, Bw. George Mandepo aliwashukuru watumishi kwa heshima hiyo na kueleza kuwa mafanikio ya Tume yanatokana na mshikamano na ushirikiano wa pamoja mahali pa kazi.
“Naipokea tuzo hii kwa unyenyekevu mkubwa. Mafanikio tunayoyaona leo ni matokeo ya kazi ya pamoja ya watumishi wote wa Tume ambao wameendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi na kujituma,” alisema Bw. Mandepo.
Aidha, aliwahimiza watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo ili kuhakikisha Tume inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kurekebisha na kuboresha sheria kwa manufaa ya Taifa.