Katibu Mtendaji Tume ya Kufekebisha Sheria Tanzania Bw. George Nathaniel Mandepo amesema kuwa utafiti ni mbinu muhimu inayoweza kusaidia Serikali kuamua kama sheria au iboreshwe au ifutwe ili kuendana na mahitaji halisi ya Taifa kwa wakati husika.
Akizungumza katika kipindi cha Morning Trumpet cha Azam Tv kinachorushwa kila siku asubuhi kiliendesha mahojiano kuhusu maendeleo ya sheria nchini, ambapo Bw. Mandepo alisema kuwa jamii inapobadilika, ni lazima sheria nazo zibadilike kulingana na hali. Mabadiliko hayo uhususha pia matokeo ya tafiti mbalimbali za Sheria zinazofanywa na Serikali hususan kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.
“Utafiti ndio unaoamua kwamba sheria itungwe, ifutwe au iboreshwe,” alisema Mandepo huku akisisitiza umuhimu wa kuihusisha Tume hiyo katika michakato muhimu ya maboresho ya sheria hapa nchini.
Alieleza kuwa tafiti husaidia kubaini changamoto zilizopo kwenye sekta husika na pia ni mbinu ambayo uhusisha wananchi wanaweza kuguswa au kuathirika kutokana na uwepo au kukosekana kwa sheria katika mbalimbali sekta kama elimu, afya, usalama barabarani na teknolojia. Utafiti hutoa mwanga kwa watunga sheria kuchukua hatua sahihi, yenye tija na husishi.
Kwa mujibu wa Mandepo, baadhi ya sheria zimekuwa zikiboreshwa kutokana na mabadiliko ya kijamii na maendeleo ya sayansi na teknolojia hapa nchini.
Alitoa mfano wa sheria za mawasiliano na matumizi ya mitandao ambazo zimekuwa zikifanyiwa marekebisho mara kwa mara kutokana na ukuaji wa teknolojia duniani.
Mathalani kwa sasa amesema,kwa maelekezo ya Serukali, Tume hiyo inaendelea na kazi ya utafiti wa mifumo ya sheria zinazoratibu matumizi ya Akili Ude (Artificial Intelligence ) na utatifi wa mifumo ya Sheria zinaohusu Biashara ya Hewa Ukaa.
Kadhalika, alieleza kuwa, miongoni mwa kazi ambazo Tume hiyo imefanya hivi karibuni ni Tathmini na Mapitio sheria za Michezo ya Kubahatisha, Sheria ya Takwimu, Sheria ya Vyama vya Ushirika, Ulinzi Mashahidi na Watoa Taarifa, Matumizi ya Shisha, Bidhaa za Tumbaku na Sigara za Kielektroniki, Sheria ya Usuluhishi pamoja na Sheria ya Makampuni na Majina ya Biashara. Pia mapendekezo ya kuboresha Sheria yametolewa kwenye Sheria za Usafirishaji Majini na Ardhini.
Aliainisha kuwa kwenye eneo ya haki jinai, Tume hiyo imepitia na kutoa mapendekezo juu ya maboresho ya sheria kwq kuzingatia matokeo ya Tume ya Rais ya Kuangalia Mifumo ya Haki Jinai (Tume ya Hakijinai). Baadhi ya Sheria zilizotazamwa ni pamoja na Sheria za Mwenendo wa Jinai, Sheria zinazogusa dhamana na Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uharifu wa Kupangwa.
Alisisitiza kuwa, kutokea kuanzishwa kwake, Tume imeweza kufanya Tafiti, Tathmini na mapitio ya Mifumo ya Sheria mbalimbali na kutoa Taarifa zaidi ya 70 zilizowezesha Serikali kuboresha sekta husika kwa kutunga, kufuta au kufanya mabadiliko kwenye sheria nyingi zinazogusa nyanja za haki madai na haki jinai, ajira, mahusiano, kazi, jamii, siasa, uchumi na maendeleo ikiwemo vivutio vya uwekezaji, mifumo ya utatuzi wa migogoro na kodi.
Tume hiyo imeendelea kutoa Elimu kwa Umma kuhusu sheria mbalimbali kwa nia ya kuwezesha wadau kufahamu haki na wajibu wao ndani ya sheria zilizopo.
Aidha, wadau wametakiwa kushiriki katika tafiti, tathmiji na mapitio ya sheria na kutoa maoni yao ili kusaidia kujenga sheria bora zinazolinda haki, usawa na maendeleo ya taifa.