Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA KUKUTANA NA MAKAMISHNA WA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA
31 Aug 2026
WAZIRI WA KATIBA NA...

DODOMA, 31 AGOSTI 2026

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, anatarajiwa kukutana na Makamishna wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kesho, Jumanne, tarehe 1 Septemba 2026.

Mkutano huo unatarajiwa kuwa fursa muhimu kwa Waziri na Makamishna kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maboresho ya sheria nchini, utekelezaji wa majukumu ya Tume pamoja na kuweka vipaumbele vya maboresho ya sheria vitakavyoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Majadiliano yanatarajiwa pia kuangazia namna mfumo wa sheria unavyoweza kuendelea kuboreshwa ili kuwa kichocheo cha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuhakikisha sheria zinaendana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi, kiteknolojia na kimazingira pamoja na mahitaji ya maendeleo ya Taifa.

Aidha, kikao hicho kitatoa nafasi kwa Waziri na Makamishna kubadilishana mawazo kuhusu changamoto, fursa na mikakati ya kuharakisha mapitio na marekebisho ya sheria, ikiwemo kubaini sheria zinazohitaji kufanyiwa maboresho ili kuweka mazingira bora ya uwekezaji na biashara, kuimarisha utawala bora na utawala wa sheria, kukuza matumizi salama ya teknolojia na ubunifu, kulinda haki na maslahi ya wananchi pamoja na kuchochea maendeleo endelevu.

Mkutano huo unafanyika wakati Serikali ikiendelea kuweka msisitizo katika kujenga mfumo wa sheria wa kisasa, unaotabirika na unaoendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ili sheria ziwe nyenzo muhimu ya kuwezesha mageuzi ya Taifa, kukuza uchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.