Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

LRCT NA LHRC ZAFANYA KIKAO CHA MASHAURIANO KUHUSU MAPITIO NA MABORESHO YA SHERIA
09 Sep 2026
LRCT NA LHRC ZAFANYA...

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) zimefanya kikao cha mashauriano kuhusu mapitio na maboresho ya sheria mbalimbali, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Maktaba ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.

Kikao hicho kiliwahusisha viongozi na wataalamu wa Tume pamoja na ujumbe wa LHRC ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt. Anna Henga. Lengo la kikao lilikuwa kujadili matokeo ya tafiti na kazi mbalimbali zilizofanywa na LHRC kuhusu sheria, pamoja na kupokea maoni na mapendekezo yatakayochambuliwa na Tume kama sehemu ya ushirikishwaji wa wadau katika utafiti, mapitio na tathmini ya sheria.

Katika kikao hicho, LHRC iliwasilisha maeneo mbalimbali ya sheria iliyoyafanyia utafiti na mapitio katika utekelezaji wa majukumu yake, pamoja na mapendekezo yanayolenga kuimarisha mfumo wa sheria, kulinda haki za binadamu, kukuza uwajibikaji na kuboresha upatikanaji wa haki.

Washiriki walijadili hoja zilizowasilishwa, wakabadilishana uzoefu na kutoa maoni kuhusu namna sheria husika zinavyoweza kuboreshwa ili ziendane na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia, pamoja na mahitaji ya wananchi na mwelekeo wa maendeleo ya Taifa.

Awali, Katibu Mtendaji wa LRCT, Bw. George Nathaniel Mandepo, na Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt. Anna Henga, walijadili umuhimu wa kuimarisha ushirikishwaji wa wadau katika mchakato wa mapitio na maboresho ya sheria, hususan katika kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Bw. Mandepo alisisitiza umuhimu wa wadau, ikiwemo LHRC, kushiriki kwa karibu katika maboresho ya sheria yanayolenga kuweka mazingira wezeshi ya kufikia matarajio ya Dira 2050. Alieleza kuwa, kutokana na nafasi ya LHRC kama mdau muhimu katika masuala ya haki za binadamu, utawala bora na upatikanaji wa haki, ushiriki wake unaweza kutoa mchango muhimu katika kuhakikisha kuwa maboresho ya sheria yanaendana na misingi na malengo ya maendeleo ya Taifa.

Aliongeza kuwa katika zoezi linaloendelea la maboresho ya sheria kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa Dira 2050, ni muhimu wadau kuendelea kutoa tafiti, uzoefu na mapendekezo yatakayosaidia kujenga mfumo wa sheria unaotabirika, wezeshi, shirikishi na unaokidhi mahitaji ya jamii, huku ukiunga mkono juhudi za Serikali za kuwaletea wananchi maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt. Anna Henga, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha sheria zinazolinda haki za binadamu, kukuza uwajibikaji, kuimarisha utawala bora na kuwezesha wananchi kupata haki kwa wakati na kwa ufanisi.

Dkt. Henga alieleza kuwa, kwa mtazamo wa LHRC, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imezingatia kwa karibu masuala ya haki za binadamu na utawala bora, ambayo ni miongoni mwa maeneo ambayo LHRC imekuwa ikiyafanyia kazi. Hivyo, taasisi hiyo ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tume na wadau wengine katika kutoa mchango unaoweza kusaidia maboresho ya sheria yanayoendana na matarajio ya maendeleo ya Taifa.

Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania za kuimarisha ushirikiano na wadau katika mchakato wa maboresho ya sheria nchini, kwa kuhakikisha kuwa tafiti, uzoefu, maoni na mapendekezo ya wadau yanapokelewa na kuchambuliwa ili kusaidia kujenga mfumo wa sheria unaoendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye ya Taifa.