Serikali imeelekeza kuanzishwa kwa utafiti wa kina kuhusu umuhimu wa kuwa na Sheria mahsusi ya Biashara Mtandao (E-Commerce Law), hatua inayolenga kuimarisha usalama, ulinzi na ufanisi wa shughuli za biashara zinazofanyika kupitia majukwaa ya kidijitali nchini.
Maelekezo hayo yametolewa leo na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, katika kikao na Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, George Nathaniel Mandepo, kilichojadili hatua zilizofikiwa katika maboresho ya sheria kwa ajili ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Katika kikao hicho, viongozi hao wamejadili kwa kina kasi ya mabadiliko ya teknolojia na kukua kwa uchumi wa kidijitali, huku ikibainika kuwa maendeleo hayo yanahitaji mfumo wa kisheria unaoendana na mazingira mapya ya biashara.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, utafiti unaopendekezwa utalenga kupitia sheria zilizopo, kubaini mapengo na changamoto za kisheria zinazohusiana na biashara mtandao, pamoja na kufanya ulinganisho wa mifumo ya sheria inayotumika katika nchi nyingine.
Hatua hiyo imekuja wakati biashara mtandao ikiendelea kukua na kuwa sehemu muhimu ya shughuli za kiuchumi, ikihusisha uuzaji na ubadilishanaji wa bidhaa na huduma kupitia teknolojia za kidijitali katika sekta mbalimbali, ikiwemo kilimo.
Majadiliano hayo yameainisha maeneo kadhaa yanayohitaji kuangaliwa katika utafiti huo, yakiwemo mikataba ya kielektroniki, ulinzi wa watumiaji, uendeshaji wa majukwaa ya kidijitali, malipo ya kielektroniki na ulinzi wa taarifa binafsi.
Maeneo mengine ni usalama wa miamala ya kielektroniki, haki miliki, kodi, ushindani pamoja na namna ya kutatua migogoro inayotokana na biashara zinazofanyika mtandaoni.
Serikali inaamini kuwa kuwa na mfumo madhubuti wa kisheria katika eneo hilo kutasaidia kujenga mazingira salama na rafiki kwa biashara na uwekezaji wa kidijitali, huku ukichochea ubunifu na ushindani miongoni mwa wafanyabiashara.
Aidha, mfumo huo unatarajiwa kuwezesha Tanzania kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa kidijitali, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Waziri Homera ameelekeza Tume ya Kurekebisha Sheria kuanzisha utafiti huo na kuandaa mapendekezo yatakayosaidia Serikali kufanya uamuzi kuhusu iwapo kuna haja ya kutungwa kwa Sheria mahsusi ya Biashara Mtandao au kufanya maboresho stahiki katika sheria zilizopo.
Hatua hiyo inaweza kuwa msingi muhimu katika kuandaa mazingira ya kisheria yanayokidhi mahitaji ya biashara za kidijitali zinazozidi kuongezeka nchini, huku ikilenga kulinda maslahi ya wafanyabiashara na watumiaji katika uchumi unaozidi kutegemea teknolojia.