Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga (Mb) amefungua Maonesho ya 5 Kitaifa ya SIDO 2026 na kulitaka Shirika hilo kuongeza juhudi katika kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kupata teknolojia na mashine za gharama nafuu zitakazowawezesha kuongeza thamani ya malighafi, kukuza biashara na kutengeneza ajira nchini.
Mhe. Kapinga aliyasema hayo tarehe 24/10/2026 katika Uwanja wa Magufuli Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wakati wa ufunguzi wa maonesho ya SIDO kitaifa 2026 ambapo alisema Tanzania ina utajiri wa rasilimali zinazotokana na Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Misitu na nyinginezo ambazo zinaweza kutumika kama msingi wa kuendeleza Viwanda na Biashara zenye tija.
Kwa upande wake Naibu Katibu wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) Bi. Zainab Chanzi alisema Tume inashiriki maonesho ya 5 Kitaifa ya SIDO kwa lengo la kutoa elimu ya sheria kwa wananchi pamoja na kupokea maoni kuhusu maboresho ya sheria mbalimbali.
Bi. Zainab alisema lengo kuu la Dira ya Taifa 2050 ni kuhahikikisha Wajasiriamali wadogo na wa kati wanajengewa mazingira wezeshi na katika kuhakikisha hilo linatimia Tume hufanya maboresho ya sheria ili kuakisi malengo ya DIRA 2050.
Aidha alieleza kuwa maonesho hayo ni fursa adhimu ya Tume kukutana na wananchi ambao ni wadau muhimu katika maboresho ya Sheria kwa kuwajengea uelewa katika maeneo mbalimbali ya sheria Tume kwa kufanya hivyo huwapa wananchi wasaa wa kutoa maoni yao jengefu yatakayosaidia katika mchakato mzima wa maboresho ya sheria na kuhakikisha sheria zinaendana na hali ya sasa ya jamii.
"Tuko hapa kutekeleza falsafa ya ushirikishwaji wa wadau kwa sababu inatupa uhalali wa kwenda kufanya maboresho ya kisheria ambayo tunaamini kwa sababu ni shirikishi yatakua yanatekelezeka kwa urahisi" alisema Bi.Zainab
Tume ya Kurekebisha Sheria inashiriki Maonesho ya 5 ya Kitaifa ya SIDO Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga yaliyoanza tarehe 20/10/2026 na kutegemewa kuhitimishwa tarehe 31/10/2026 kwa lengo la kutoa elimu ya sheria kwa Umma.