Watumishi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ambao ni Wasimamizi wa Vihatarishi (Risk Champions) wanaohusika na uhuishaji wa Daftari la Vihatarishi, wametakiwa kutoa ushirikiano kwa wataalamu wawezeshaji, na kushiriki kikamilifu katika majadilianona kuhakikisha kuwa nyaraka zitakazoandaliwa zinaakisi mazingira halisi ya utekelezaji wa majukumu ya Tume.
Wito huo umetolewa tarehe 19 Oktoba 2026 katika ukumbi wa Sunset Hotel mkoani Iringa ambapo kikao kazi cha Siku nne kinafanyika kwa wasimamizi wa vihatarishi (Risk Champions) wa Tume hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi (DCS) Bw. Mohamed Mavura, alisema kikao kazi cha kuhuisha Daftari la vihatarishi katika Tume hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Waraka Na. 12 wa Mwaka 2013 uliotolewa na Wizara ya Fedha unaoelekeza pamoja na masuala mengine, Taasisi za Umma kufanya Tathmini ya Vihatarishi (Risk Assesment) kila mwaka na kuandaa Daftari la Vihatarishi (Risk Register) pamoja na mpango kazi wa utekelezaji wa hatua za kudhibiti Vihatarishi.
Aidha Bw. Mavura alisema lengo la kikao hicho ni kuimarisha Usimamizi wa Vihatarishi ili kuiwezesha Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kufikia malengo ya kimkakati na kitaasisi.
“Kikao hiki kinalenga kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa hatua za kudhibiti Vihatarishi, ukianisha majukumu, muda wa utekelezaji na viashiria vya ufuatiliaji” alisema Bw. Mavura
Kwa upande wake Mwezeshaji katika kikao kazi hicho ambaye ni Mkaguzi kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa ndani wa Serikali Bw. Felix Kapesula, alisema kujua Vihatarishi wakati watumishi wanatekeleza majukumu yao husaidia kufanya maamuzi sahihi na kusisitiza kuwa utaratibu huo unafanya kuongezeka kwa kuaminika shughuli za Taasisi kwa wadau wa maendeleo.
Kikao kazi cha kuhuisha Daftari la Vihatarishi la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania mwaka 2026/2027 kimeanza leo tarehe 19 Ocktoba 2026 kikitegemewa malizika ifikapo tarehe 22 oktoba 2026 mkoani Iringa.