Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

WAZIRI HOMERA AITAKA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA KUSHIRIKISHA WADAU KATIKA MAPITIO YA SHERIA.
01 Sep 2026
WAZIRI HOMERA AITAKA...

Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Juma Homera, ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kushirikiana kwa karibu na wadau wa sekta ya sheria, wakiwemo Mawaziri wa kisekta, katika kupata maoni na mapendekezo wakati wa mapitio ya mifumo mbalimbali ya sheria nchini.

Homera ameyasema hayo leo, Septemba 1, 2026, mjini Dodoma wakati akifungua kikao cha mafunzo elekezi kwa makamishna wapya wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Grewill, Jijini Dodoma.

Waziri Homera amesema ushirikishwaji wa wadau hao ni muhimu katika kuhakikisha maboresho ya sheria yanaendana na mahitaji halisi ya jamii na yanawezesha Tanzania kutekeleza kwa ufanisi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amesema Tume inapaswa kutumia nafasi yake kuendelea kufanya mapitio ya sheria na mifumo ya kisheria kwa kuzingatia mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia yanayoendelea nchini.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kupata maoni, ukosoaji na mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali ili kuhakikisha sheria zinazopendekezwa kwa maboresho zinakuwa na tija na zinakidhi mahitaji ya Taifa.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, George Mandepo, amesema uwepo wa makamishna wenye weledi wa hali ya juu umeongeza uwezo na ufanisi wa Tume katika kutekeleza majukumu yake.

Mandepo amesema uzoefu na utaalamu wa makamishna hao walioteuliwa utaiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi, hususan katika kufanya tafiti, kupitia sheria mbalimbali na kutoa mapendekezo ya maboresho ya sheria nchini.

Amesema Tume itaendelea kutumia weledi na uzoefu wa makamishna wake katika kuhakikisha inatimiza kwa ufanisi wajibu wake wa kusaidia kuboresha mfumo wa sheria nchini.

Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Tume na wadau wa sekta ya sheria ni muhimu katika kujenga mfumo wa sheria unaoendana na mahitaji ya sasa na matarajio ya maendeleo ya Tanzania.