Wanafunzi wa Shule za Mkoani Shinyanga ambazo ni Old Shinyanga High School na na Uhuru Sekondari zimepata fursa ya kupata elimu ya Sheria ya Michezo ya Kubahatisha na athari zitokanazo na kujihusisha na michezo hiyo kwa wanafunzi.
Elimu hiyo imetolewa April 14,2026 na maafisa kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ambao walifika katika shule hizo na kuzungumza na wanafunzi hao.
Akizungumza na wanafunzi hao Naibu Katibu ambae pia ni mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Sheria kwa Umma kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bi. Zainab Chanzi alisema kuwa Tume imefanya Tathmini kuhusu Sheria ya Michezo ya Kubahatisha , na kwa mujibu wa tathmini hiyo imebainika kuwapo kwa kundi kubwa la wanafunzi kushiriki michezo hiyo jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura 41. Kwa mujibu wa Sheria hiyo ni marufuku kwa mtoto wa chini ya miaka 18 kucheza michezo ya Kubahatisha, ili kulinda ustawi wa mtoto katika jamii.
“athari ni kubwa zaidi kwa wanafunzi ndio maana Sheria imezuia msishiriki michezo hiyo, wengine mtakosa kuzingatia masomo, mtatumia fedha za ada kubeti na hata wengine kutoroka shule au kutoingia madarasani” alisema Naibu Katibu Bi Zainab.
Aliongeza kwa kueleza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inasisitiza kujiandaa kuingia katika Uchumi lmara, Jumuishi na Shindani na hilo litawezekana iwapo tutaandaa jamii iliyostaarabika na yenye weledi hususan kwa kizazi kijacho ambacho kinajumuisha wanafunzi ambao ndio sehemu ya Taifa la kesho linalotarajiwa.
Awali Afisa Sheria wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ,Richard Mdee alibainisha madhara ya kushiriki kwa mwanafunzi katika michezo ya kubahatisha kuwa ni pamoja na kuathirika kisaikolojia,akisisitiza hali hiyo hutokea zaidi pale mwanafunzi anapocheza na kuliwa kiasi cha pesa alichotajaria kukizalisha kwa michezo hiyo,pia kuongezeka kwa tabia hatarishi hususan mazingira ya shuleni.
“Vitendo vya wizi na udokozi ni rahisi kutokea pindi mwanafunzi anaposhiriki michezo ya kubahatisha na akakosa fedha uwezekano wa kuiba hata viatu vya wanafunzi wenzie akauze ili apate fedha ya kubeti hapo ndipo hatari inaweza kutokea zaidi” alisema Richard.
Afisa huyo aliongeza kwa kueleza kuwa kwa mujibu wa kifungu namba 50 na 74 vya Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura ya 41 inatoa adhabu kwa mtu au kampuni itakayomshirikisha mtoto moja kwa moja kwenye masuala ya michezo ya kubahatisha na kwamba itakapothibitika muhusika atatozwa faini isiyopungua million moja na isiyozidi milioni tano.
Kwa upande wake Mwalimu Sylvester Kalwinji wa Shule ya Sekondari Uhuru, alisema kuna kundi kubwa la watoto wanaoshiriki michezo hiyo na wamiliki au wachezeshaji wa michezo hiyo wanawachukulia wanafunzi kama ni sehemu ya wateja kitu ambacho ni kiyume na Sheria.
“Tunawaomba hata wazazi waweze kupewa elimu hii ili watusaidie kuwazuia watoto wasishiriki michezo hiyo kwani inapoteza ufanisi wao katika masomo ” alieleza mwalimu huyo.
Sambamba na hilo wanafunzi Mariam Wilson wa shule ya sekondari Uhuru na Dickson Matiku wa shule ya sekondari Old Shinyanga wamesema elimu juu ya michezo ya kubahatisha imewafumbua na kwamba wengi wao hawakujua kwamba michezo ya kubahatisha hairuhusiwi kuchezwa na watoto chini ya miaka 18 na kuhaidi kuwa mbalozi wema kwa jamii ili kujenga jamii bora.
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inaedelea na zoezi utoaji elimu ya sheria kwa umma kupitia mikutano mbalimbali na wanafunzi katika mkoa wa Shinyanga ili kujenga jamii yenye uelewa kuhusu masuala ya kisheria.