Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

WAJASIRIAMALI KAHAMA WAIOMBA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA KUPITIA UPYA SHERIA ZA KODI NA TOZO.
29 Oct 2026
WAJASIRIAMALI KAHAMA...

Wajasiriamali walioshiriki katika Maonesho ya SIDO Kitaifa 2026 yaliyofanyika katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, wameiomba Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kuangalia upya sheria zinazohusu kodi na tozo mbalimbali zinazotozwa na Taasisi za Umma, ili kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na kuwawezesha kukuza mitaji yao.

Wajasiriamali hao wameeleza kuwa uwepo wa tozo kutoka Taasisi mbalimbali, zikiwemo Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Halmashauri na Taasisi nyingine, kunawaongezea gharama na kutumia muda mwingi katika kutimiza matakwa ya kisheria yanayohusiana na shughuli zao za biashara.

Kutokana na hali hiyo, wamependekeza kuwepo kwa mfumo jumuishi wa utoaji huduma na usimamizi wa tozo, ambapo wajasiriamali wataweza kupata huduma zinazohitajika kupitia kituo kimoja, hatua wanayoamini itasaidia kupunguza urasimu, gharama na muda unaotumika kufuata taratibu za taasisi mbalimbali.

Maombi hayo yametolewa Oktoba 28, 2026, baada ya mawakili wa serikali kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Bi. Vicky Mbunde na Bw. Richard Mdee, kutoa elimu ya sheria kwa wajasiriamali hao kuhusu majukumu ya Tume hiyo pamoja na haki na wajibu wa mtuhumiwa.

Katika mada zao, Mawakili hao wameeleza masuala yanayohusu uelewa wa sheria na umuhimu wa wananchi kuzifahamu haki na wajibu wao ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kuzingatia sheria zilizopo nchini.

Wajasiriamali hao wameeleza kuwa kupitia upya sheria na taratibu zinazohusu kodi na tozo kunaweza kusaidia kuweka mazingira rafiki zaidi ya biashara, hususan kwa wajasiriamali wadogo ambao mara nyingi hukabiliwa na changamoto za mitaji na gharama za uendeshaji.

Aidha, wajasiliamali hao wameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kuzingatia maoni na changamoto wanazokutana nazo wajasiliamali katika shughuli zao za kila siku, ili mapendekezo ya marekebisho ya sheria yaendane na mahitaji halisi ya wananchi na kuchochea ukuaji wa biashara ndogo na za kati.

Wamesisitiza kuwa mfumo unaorahisisha taratibu za kisheria na kiutawala unaweza kusaidia kuongeza ufanisi katika biashara, kukuza uzalishaji, kuongeza ajira na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Akijibu hoja za wajasiriamali hao Bi Vicky Mbunde ameeleza kwamba malalamiko yao wameyachukua na kuahidi kwamba yatafika sehemun husika ili kufanyiwa kazi.

Aidha  Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inaendelea kutoa elimu ya sheria kwa umma ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu sheria, haki na wajibu wao, pamoja na kukusanya maoni yanayoweza kusaidia kuboresha sheria na mifumo ya utoaji haki nchini.