Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

LRCT WAKUSANYA MAONI KUHUSU UTAFITI WA NAMNA BORA YA KUPINGA MAAMUZI YA KIUTAWALA MAHAKAMANI
03 Nov 2026
LRCT WAKUSANYA MAONI...

Dodoma, Novemba 3,2026

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imefanya kikao na wadau cha kukusanya maoni ya Utafiti kuhusu  Namna Bora ya Kupinga Maamuzi ya Kiutawala Mahakamani.

Kikao hicho kimefanyika tarehe 3/11/2026 katika ukumbi wa Rafiki Hotel iliyopo Jijini Dodoma ambapo wadau kutoka Wizara, Idara na Tasisi mbali mbali wameshiriki kutoa maoni yao.

Akizungungumza wakati wa kikao hicho Naibu -  katibu Idara ya Utafiti kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bi. Juliana Munisi alisema chimbuko la Utafiti huo ni Maelekezo kutoka kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Alieleza kuwa maelekezo hayo yalitokana na mijadala iliyokuwa inaendelea Bungeni hususan katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ambayo ilibaini uwepo wa mkanganyiko katika mfumo wa Sheria za kupinga maamuzi ya kiutawala ambapo baadhi ya sheria maamuzi hayo hupingwa kwa kutumia utaratibu wa Mapitio ya Kimahakama, kwa njia ya rufaa na huku sheria nyingine zikizuia kupinga maamuzi hayo. 

Aidha, imeelezwa kuwa msingi wa maelekezo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali unatokana na masharti ya kifungu cha 80 (2) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura ya 263 kinachotoa haki kwa mtu asiyeridhika na maamuzi ya Waziri mwenye dhamana na masuala ya kazi  kukata rufaa Mahakama Kuu.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kupitia kifungu hicho alibaini kuwa sambamba na Sheria hiyo,  kuna Sheria mbalimbali nchini zilizoainisha masharti tofauti kuhusu utaratibu wa kupinga maamuzi ya kiutawala.

"Hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitoa maelekezo kwa Tume kufanya utafiti na kupendekeza namna bora ya kupinga maamuzi ya kiutawala mahakamani."
alisema Bi. Juliana.

Aidha, Bi. Juliana alieleza kuwa maboresho ya Sheria hizo ni sehemu ya utekelezaji wa Dira 2050 ambayo pamoja na masuala mengine inasisitiza Utawala bora na Utawala wa sheria.
Hivyo ili kufikia malengo ya Dira hiyo, Sheria zilizopo zinapaswa kuwa wezeshi zinazotoa nafasi  kwa kila mdau na mamlaka kutelekeza majukumu yake kwa kuzingatia misingi iliyowekwa na sheria.

Katika kutoa maoni kuhusu utafiti huo, baadhi ya wadau  walioshiriki kikao hicho  walieleza kuwa Sheria zinapaswa kuwa wazi kuhusu hatua za kufuatwa wakati wa kupinga maamuzi ya kiutwala, ikiwemo kuweka ukomo wa kusikiliza mashauri, namna ha kusikiliza mashauri, na utaratibu wa kuandaa taarifa za mwenendo wa mashauri. Wadau hao walieleza kuwa kubainisha masuala hayo katika sheria kutasaidia kuondoa changamoto iliyopo sasa kwa baadhi ya mamlaka kutoa maamuzi bila kuzingatia misingi ya haki ya asili, na kutotoa uamuzi kwa wakati na kufata taratibu za utaoaji wa maamuzi.

Sambamba na hayo wadau pia walieleza kuwa taratibu zilizopo za kupinga Maamuzi ya kiutawala zinapaswa kufafanuliwa kwa uwazi ili kuwasaidia wahusika kufahamu utaratibu wa kisheria uliopo.
Mfano, Mamlaka zinazotekeleza majukumu yanayofanana au sekta zinazofanana zinaweza kuwekewa utaratibu wa aina moja kulingana na aina ya mamlaka muundo wake ili kurahisisha utaratibu wa upingaji wa maamuzi yatakayotolewa na mamlaka au taasisi husika

Hadi sasa Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania imebaini zaidi ya Sheria 42 zenye uhitaji wa maboresho yatakayowezesha  kuweka namna bora ya kupinga maamuzi ya kiutawala Mahakamani ambapo Utafiti wake unaendelea.