Timu ya watafiti kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania leo imekutana na baadhi ya wenyeviti, madiwani pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Tarime DC), kwa lengo la kukusanya maoni kuhusu Mfumo wa Sheria wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (Corporate Social Responsibility – CSR) na Ushirikishwaji wa Wananchi katika Matumizi ya Rasilimali.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiiyo kiliongozwa na Naibu Katibu wa Idara ya Utafiti wa Tume hiyo, Bi. Juliana Munisi, ambapo washiriki wamepata fursa ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uwajibikaji wa kampuni kwa jamii na namna wananchi wanavyoshirikishwa katika matumizi ya rasilimali za ndani na mchango wa kampuni katika maendeleo ya jamii za maeneo zinakofanyia shughuli zake.
Katika majadiliano hayo, washiriki wametoa maoni, mapendekezo na uzoefu wao kuhusu changamoto zilizopo katika utekelezaji wa mfumo wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii.
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inaendelea kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali, ambao ni mamlaka za Serikali za Mitaa, wataalamu na wananchi yatakayosaidia kuboresha mfumo wa uwajibikaji wa kampuni kwa jamii na ushirikishwaji wa wazawa.
Tume inaendelea kutoa nafasi kwa wadau kushiriki katika mchakato huo ili kuhakikisha mapendekezo ya maboresho ya sheria yanazingatia maslahi ya wananchi.