Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) imekutana na ujumbe wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) kujadili namna bora ya kupinga maamuzi ya kiutawala kupitia mahakama, ikiwa ni sehemu ya utafiti wa Tume unaolenga kubaini changamoto zilizopo katika mfumo wa sheria na kupendekeza maboresho yatakayorahisisha upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Kikao hicho, kilichoratibiwa na Tume, kimefanyika tarehe 5 Novemba 2026 katika ukumbi wa mikutano wa OCPD jijini Dodoma, kikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Uandishi wa Sheria, Bi. Chresencia Mathayo, kwa niaba ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, huku ujumbe wa Tume ukiongozwa na Mkuu wa Idara ya Utafiti, Bi. Juliana Munisi.
Katika kuwasilisha muktadha wa utafiti huo, Tume imeeleza kuwa maamuzi ya kiutawala yana msingi wake katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na sheria mbalimbali, hata hivyo, sheria hizo zinatofautiana katika kuweka utaratibu wa kupinga maamuzi hayo, ambapo baadhi hazibainishi njia za kufuata huku nyingine zikiweka vizuizi vya kuyapinga, hali inayoonesha umuhimu wa kuchunguza na kuoanisha masharti yaliyopo.
Akifafanua hilo Bi. Munisi amesema, “Kwa mfano sheria nyingine zinatoa utaratibu wa kupinga maamuzi ya kiutawala kwa njia ya rufaa na nyingine kwa njia ya mapitio”
Akichangia katika majadiliano hayo, Bi. Mathayo ameihimiza Tume kuchunguza namna ya kuimarisha mifumo ya utatuzi wa migogoro ndani ya mamlaka za kiutawala ili kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani, huku akisisitiza umuhimu wa sheria kubainisha wazi njia za kupinga maamuzi hayo na kupendekeza marekebisho pale ambapo vifungu vinavyoondoa mamlaka ya mahakama kusikiliza mashauri vinakinzana na masharti ya Katiba.
Aidha, utafiti huo unalenga kutathmini iwapo mfumo uliopo unakidhi viwango vya utawala bora na kuwezesha upatikanaji wa haki, pamoja na kubaini changamoto za kisheria na kiutendaji zinazoukabili, ambapo matokeo yake yatatumika kuandaa mapendekezo ya kuweka uwiano katika sheria ili wananchi waweze kutambua mamlaka wanayopaswa kuwasilisha mashauri yao, taratibu za kufuata na nafuu za kisheria wanazoweza kuomba.