Shinyanga, Oktoba 30, 2026
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeendelea na kampeni yake ya kutoa elimu ya sheria kwa umma katika Mkoa wa Shinyanga, kwa kutoa elimu kuhusu makosa ya utakasishaji fedha haramu kupitia kituo cha redio cha Faraja FM 91.1.
Elimu hiyo imetolewa leo, Oktoba 30, 2026, na Mawakili wa Serikali kutoka Tume hiyo, Bi. Vicky Mbunde na Bw. Richard Mdee, kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuelewa sheria ya Utakatishaji fedha Sura ya 243, maana ya utakasishaji, vitendo vinavyohusiana na kosa hilo na kufahamu athari zake kisheria.
Kupitia kipindi hicho, wananchi wamepata fursa ya kujifunza umuhimu wa kuzingatia sheria katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii, pamoja na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhusishwa na utakasishaji fedha haramu.
Akizungumza katika kipindi maalum cha redio hiyo Wakiki Vicky Mbunde amesema Kampeni hiyo ni sehemu ya jitihada za Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania za kuimarisha uelewa wa sheria kwa wananchi, ili waweze kutambua wajibu wao, kufanya maamuzi sahihi na kuepuka kujihusisha na vitendo vinavyokiuka sheria.
"Utakasishaji wa fedha haramu ni kosa la kisheria linaloweza kuathiri uchumi na usalama wa jamii. Kila mwananchi ana wajibu wa kutambua, kuepuka na kutoa taarifa kuhusu vitendo vinavyohusiana na utakasishaji fedha haramu ili kulinda uchumi wa taifa na kuimarisha utawala wa sheria.” Vilevile kosa la utakatishaji fedha adhabu yake ni kifungo miaka ishirini au faini milioni mia moja na isiyopungua milioni miatano au faini mara tatu ya faida iliyopatikana na fedha haramu alisema Vicky
Kwa upande wake Wakili Richard Mdee alieleza kwamba Jamii inaweza kujihusisha na utakatishaji wa fedha haramu kwa kujua au bila kujua, kupitia kupokea, kuhifadhi, kuhamisha au kutumia fedha zinazotokana na shughuli za uhalifu.
Aidha aliongeza kwamba kila mwanajamii ana wajibu wa kujiepusha na makosa ya utakatishaji wa fedha haramu kwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili kulinda uchumi na usalama wa taifa.
Tume inaendelea kutumia vyombo mbalimbali vya habari, ikiwemo redio, kufikisha elimu ya sheria kwa wananchi katika maeneo tofauti nchini, kwa lengo la kuongeza uelewa wa sheria na kuhamasisha jamii kuishi kwa kufuata sheria na taratibu za nchi.