Dodoma.
Viongozi wa taasisi za umma na binafsi nchini wametakiwa kuwa na uelewa wa masuala ya usalama wa mtandao ili kuimarisha ulinzi wa taarifa, mifumo ya kidijitali na mali za taasisi wanazoziongoza, huku wakitakiwa kutambua kuwa jukumu hilo si la wataalamu wa TEHAMA pekee.
Wito huo umetolewa leo Novemba 13, 2026, jijini Dodoma na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Dkt. Eliamani Laltaika, wakati wa kikao cha kukusanya maoni ya wadau kuhusu mfumo wa sheria zinazosimamia matumizi ya Akili Unde.
Dkt. Laltaika amesema mabadiliko ya teknolojia yameongeza umuhimu wa viongozi kuwa na uelewa wa usalama wa mtandao, kutokana na taasisi nyingi kumiliki taarifa muhimu za serikali na mali zinazohifadhiwa kwenye mifumo ya kidijitali.
Amesema kwa sasa uelewa wa masuala ya usalama wa mtandao umekuwa miongoni mwa vigezo vinavyozingatiwa katika usaili wa watumishi wanaopandishwa vyeo au kuteuliwa kushika nafasi za ukurugenzi.
"Haikubaliki tena kiongozi wa taasisi kutojua usalama wa mtandao," amesema Dkt. Laltaika, akibainisha kuwa baadhi ya nchi, zikiwemo Kenya na Rwanda, zimeweka matakwa ya lazima kuhusu uelewa wa masuala hayo.
Ameeleza kuwa usalama wa mtandao hauhusu teknolojia pekee, bali pia unajumuisha mifumo ya kisheria, kijamii na kiuchumi inayolenga kuhakikisha watumiaji wanakuwa salama wanapotumia teknolojia za kidijitali.
Amebainisha kuwa usalama huo unahusisha maeneo makuu matatu ambayo ni vifaa (Hardware), programu (Software) na maudhui (Content), hivyo kuwepo kwa ulinzi katika maeneo hayo ni muhimu katika kukabiliana na vitisho vya mtandaoni.
Katika hatua nyingine, Dkt. Laltaika ameonya kuwa nchi zinaweza kukabiliwa na mashauri ya kisheria kutokana na kushindwa kuweka sheria na mifumo madhubuti ya kusimamia matumizi ya Akili Unde.
Ametolea mfano shauri lililofunguliwa nchini Kenya dhidi ya serikali, Mwanasheria Mkuu, Bunge na taasisi nyingine za umma, kwa madai ya matumizi ya Akili Unde bila kuwepo kwa mfumo wa kutosha wa kisheria.
Amesema Tanzania nayo inaweza kukabiliwa na changamoto zinazofanana, ikiwemo katika mahakama za kikanda, iwapo haitachukua hatua za mapema kuweka mazingira ya kisheria yanayoendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, George Mandepo, amesema utafiti unaofanywa na Tume hiyo unalenga kubaini mapungufu yaliyopo katika sheria na mifumo ya kitaasisi inayohusiana na matumizi ya teknolojia, pamoja na kupendekeza hatua stahiki za kuchukuliwa.
Amezitaja sheria zinazohusiana na teknolojia na taarifa za kielektroniki kuwa ni Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta, Sheria ya Makosa ya Mtandao, Sheria ya Ushahidi, Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania na Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.
Amesema kasi ya maendeleo ya Akili Unde imeibua umuhimu wa kufanya tathmini ya sheria hizo ili kubaini kama zinatoa msingi wa kutosha wa kusimamia matumizi ya teknolojia hiyo au kama kuna mianya inayoweza kusababisha ukiukwaji wa sheria na haki za wananchi.
Ameongeza kuwa tathmini hiyo itazingatia masuala ya uwajibikaji, uwazi katika maamuzi yanayotolewa na mifumo ya Akili Unde, usalama wa taarifa na namna ya kuweka uwiano kati ya kukuza ubunifu wa kiteknolojia na kulinda maslahi ya umma.
Mandepo amesisitiza kuwa lengo la mfumo wa kisheria unaopendekezwa si kuzuia maendeleo ya teknolojia, bali kuhakikisha matumizi yake yanafanyika kwa kuzingatia sheria, maadili na haki za binadamu.
"Dhamira yetu si kuzuia maendeleo katika sekta ya sayansi, bali kuhakikisha yanafanyika ndani ya mfumo wa sheria unaolinda haki," amesema.
Amefafanua kuwa mfumo huo unatarajiwa kuzingatia misingi ya uwazi, maadili, uwajibikaji, usalama, faragha, usawa, ujumuishi na ulinzi wa haki za binadamu.
Aidha, amesema kwa kuwa Akili Unde ni teknolojia mtambuka inayogusa takribani sekta zote, ni muhimu sheria zitakazowekwa kuangalia kwa mapana athari na manufaa yake kwa taifa.
Amebainisha kuwa changamoto zinazokabili nchi zinazoendelea katika kusimamia teknolojia si ukosefu wa sheria pekee, bali pia ni pamoja na sheria kugongana, udhaifu wa mifumo ya usimamizi, changamoto za kifedha na uwepo wa taasisi nyingi zinazoshughulikia eneo moja.
Amewataka wadau kutoka sekta za umma na binafsi, wizara, taasisi za elimu, watafiti na wataalamu wa TEHAMA kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yatakayoiwezesha Tume kuandaa mapendekezo yenye tija na yanayoweza kutekelezwa na Serikali.