Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

WADAU SHINYANGA WANUFAIKA NA ELIMU YA SHERIA MBALIMBALI KUHUSU MAKOSA YA JINAI.
18 Apr 2026
WADAU SHINYANGA WANU...

Wadau Shinyanga wanufaika na elimu ya sheria mbalimbali kuhusu makosa ya jinai iliyotolewa na maafisa kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ili kuwasaidia wananchi hao kujua haki na wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kukusanya maoni katika maeneo mbalimbali yenye changamoto za kisheria.

Akizungumza na wadau hao wakati wa utoaji wa elimu hiyo tarehe 16 Aprili 2026 katika ukumbi wa Ofisi  ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Naibu Katibu kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bi. Zainab Chanzi, alisema licha ya elimu hiyo kuwasaidia wananchi kujua haki na wajibu wao kisheria lakini pia ni utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai iliyopendekeza wananchi kupewa elimu kuhusu masuala ya jinai ili wajue haki na wajibu wao kisheria na kuboresha mfumo wa utoaji haki nchini.

Aidha Bi.Zainab aliendelea kuwa kutokana na mapendekezo hayo Tume ya Kurekebisha Sheria imekua ikitoa elimu katika maeneo ambayo yanaonesha kuwapo kwa changamoto ya  uelewa kwa wananchi ikiwemo   elimu kuhusu dhamana , masharti ya dhamana ili kusaidia jamii kuelewa kuwa dhamana ni haki kisheria  iwapo mtuhumiwa amekidhi vigezo na masharti na kosa husika lina dhamana kwa mujibu wa Sheria.

Sambamba na hilo, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imetoa elimu kuhusu Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Haki za Mshtakiwa katika Makosa ya Jinai  na Wajibu wa Mkopaji na  Mkopeshaji. Suala la mikopo kwa sasa limekua lina changamoto mathalani wakopaji kuwa na uelewa mdogo kwenye  kiwango cha riba, muda wa marejesho, dhamana ya mkopo na namna mkopeshaji anavyotakiwa kudai deni lake.

Elimu hii imetolewa kwa makundi makundi mbalimbali ikiwemo watendaji wa kata, mtaa,wajasiliamali, madereva wa bodaboda na bajaji , watu wenye ulemavu pamoja na viongozi wa dini ili waweze kuwa mabalozi wazuri katika  maeneo yao.

Mmoja kati ya wanufaika wa elimu hiyo Askofu Emmanuel Joseph Makala ambae pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Amani na Maridhiano Mkoa wa Shinyanga, alisema jamii inahitaji kujifunza mara kwa mara juu ya sheria zilizopo na kuhimiza waliopata elimu hiyo kuifikisha kwa jamii ili kusaidia kujiepusha na kutenda makosa kinyume na Sheria.

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inaendelea kutekeleza jukumu lake kutoa elimu ya sheria kwa jamii, kuhusu marekebisho mbali mbali ya Sheria kupitia vikao na wadau katika mikoa ya Shinyanga, Tabora, Tanga na Morogoro.