Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

WAAJIRIWA WAPYA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA WAPATIWA MAFUNZO ELEKEZI
12 May 2026
WAAJIRIWA WAPYA TUME...

Waajiriwa wapya wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania wameanza rasmi mafunzo elekezi (orientation course) yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, mafunzo yanayotolewa na wataalamu kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.

Mafunzo hayo yanafanyika kwa lengo la kuwajengea uwezo watumishi hao wapya katika misingi ya utumishi wa umma, yamefunguliwa rasmi leo tarehe 04.05.2026 na Kaimu Katibu Mtendaji Tume hiyo, Bw. Burhani Kishenyi, ambaye aliwataka washiriki kuyachukulia kwa uzito ili waweze kutoa mchango chanya katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza wakati wa ufunguzi, Bw. Kishenyi alisema kuwa Tume ina jukumu muhimu la kupitia na kuboresha sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ili ziendane na mahitaji ya jamii na mabadiliko ya wakati, hivyo ni muhimu kwa watumishi wapya kuelewa kwa kina majukumu yao pamoja na maadili ya kazi.

“Tunategemea kuona mabadiliko chanya kupitia utendaji wenu ambapo mafunzo haya ni msingi muhimu wa kuwajenga kitaaluma na kiutendaji,” alisema.

Aidha Bw. Kishenyi alisema kwamba  mafunzo hayo yatawapatia ujuzi na uelewa juu ya namna bora ya kufanya Mawasiliano na Umma/Jamii/Wadau wa Tume kwa kuwa ndio watakaokutana nao mara kwa mara katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

“Tume tunakutana na wananchi na wadau wetu kwa njia mbalimbali katika utendaji wetu wa kazi.  Kazi hizi za mawasiliano na Umma zinahitaji tuwe na weledi juu ya namna ya kuzungumza na Umma na jamii tunazowasiliana nazo” alisema.

 Kwa upande wake Mkurugenzi wa chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Singida Dkt. Emmanuel Tandika , alisema  kuwa mafunzo hayo yanajumuisha mada mbalimbali ikiwemo maadili ya Utumishi wa Umma, mbinu za utendaji kazi, uwajibikaji pamoja na usimamizi wa sheria na taratibu za Serikali.

Naye Bw. Mathew Kilasi Mratibu wa mufunzo kutoka chou hicho  alieleza kwamba watajifunza kuhusu misingi ya uongozi bora, uwajibikaji, utoaji wa huduma  kwa umma pamoja na umuhimu wa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi hivyo ni muhimu watumishi kuzingatia mafunzo hayo ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Awali akiwakaribisha wakufunzi hao na watumishi kwa ujumla Mkuu wa Sehemu ya Usimzmizi wa Rasilimali watu na Utawala Bw. Ambokile Mwakasungula alieleza kuwa mafunzo hayo yatatolewa kwa muda wa siku tatu kuanzia leo tarehe 04 mpaka tarehe 06, 2026 ambapo alieleza kwamba yatawasaidia watumishi kuelewa muundo wa Tume, majukumu na taratibu za kiutumishi pamoja na maadili ya kazi.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na mpango huo, wakisema utawasaidia kuanza kazi zao wakiwa na uelewa mpana wa mazingira ya utumishi wa umma na matarajio ya Taasisi na Taifa kwa ujumla.