Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeendelea kujiimarisha katika utekelezaji wa majukumu yake kwa kuwajengea uwezo watumishi wake kupitia mafunzo kuhusu mfumo wa sheria zinazosimamia sekta ya nishati, hususan petroli na gesi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mafunzo hayo yametolewa na mtaalamu wa sheria za nishati, Dk. Boniface Luhende, katika ukumbi wa Hoteli ya APC Bunju jijini Dar es Salaam, yakilenga kuongeza uelewa kuhusu mifumo ya kisheria, sera na kanuni zinazosimamia rasilimali za petroli na gesi nchini.
Akitoa mada katika mafunzo hayo, Dk. Luhende alisema kuwa sekta ya nishati inatarajiwa kuwa miongoni mwa sekta muhimu zitakazochochea maendeleo ya uchumi wa Tanzania katika kipindi cha utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na mfumo wa sheria unaoendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Alieleza kuwa maendeleo ya teknolojia, mabadiliko ya mazingira ya uwekezaji na mahitaji ya wananchi yanahitaji mapitio ya mara kwa mara ya sheria ili kuhakikisha zinatoa mwongozo stahiki katika usimamizi wa rasilimali za petroli na gesi kwa manufaa ya taifa.
“Dira ya Taifa 2050 inahitaji uwepo wa mifumo madhubuti ya kisheria itakayowezesha matumizi bora ya rasilimali za nishati, kuvutia uwekezaji, kulinda mazingira na kuhakikisha Watanzania wananufaika na rasilimali zao,” alisema Dk. Luhende.
Kwa upande wake Profesa Saudin Jacob Mwakaje amesema kuwa mafanikio ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanategemea uwepo wa mfumo madhubuti wa sheria zinazosimamia uwekezaji nchini.
Akiwasilisha mada kuhusu mfumo wa kisheria wa uwekezaji Tanzania, alieleza kuwa sheria zinapaswa kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na kutoa mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje.
Prof. Mwakaje alisisitiza umuhimu wa uwazi katika mikataba ya uwekezaji, ulinzi wa haki za wawekezaji, pamoja na usimamizi bora wa migogoro ya kibiashara ili kuongeza imani ya wawekezaji.
Aidha alibainisha kuwa Dira 2050 inalenga kujenga uchumi wa kisasa unaoongozwa na sekta binafsi, hivyo maboresho ya sheria na taasisi za uwekezaji ni jambo la msingi katika kufikia malengo hayo.