Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imewakumbusha wenyeviti wa mabaraza ya kata kwamba wasiwe wanyonge katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa kuwa sheria inawatambua na imewapa mamlaka ya kutekeleza sheria ya mabaraza ya kata. Hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Akizungumza leo tarehe 15/04/2026 katika kikao cha utoaji elimu ya sheria kilichofanyika mkoani Tanga, Bi. Vicky Mbunde Wakili kutoka Tume hiyo alisema bado kuna baadhi ya viongozi wa mabaraza ya kata ambao hawana uelewa wa kutosha kuhusu mamlaka yao kisheria, hali inayoweza kuathiri utendaji wao katika utiaji haki.
“Sheria inawatambua wenyeviti wa mabaraza ya kata kama sehemu muhimu ya mfumo wa utoaji haki katika ngazi ya kata. Ni wajibu wao kuhakikisha wanasimamia haki kwa usawa na kuzingatia taratibu zote za kisheria,” alisema.
Aidha, Mbunde aliongeza kuwa mabaraza ya kata yana nafasi kubwa katika kusuluhisha migogoro ndani ya kijamii ikiwemo ya migogoro ya ardhi, ndoa na madai, hivyo viongozi wake wanapaswa kuwa waadilifu na katika kusimamia misingi ya haki.
Kwa upande wao, baadhi ya wenyeviti wa mabaraza ya kata waliohudhuria kikao hicho walikiri kuwa elimu hiyo imewasaidia kufahamu vyema mipaka ya mamlaka yao pamoja na namna bora ya kushughulikia mashauri yanayowasilishwa mbele yao.
“Tumeelewa kuwa tunapaswa kufuata sheria kikamilifu na kutoa maamuzi ya haki bila upendeleo. Hii itasaidia kuongeza imani ya wananchi kwetu,” alisema mmoja wa wenyeviti hao. Vick Mbunde ameeleza kuwa TUME itaendelea kutoa elimu kwa viongozi wa ngazi za chini ili kuimarisha utendaji kazi wa vyombo vya utatuzi wa migogoro na kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi kwa urahisi zaidi.