Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA YATOA ELIMU YA SHERIA KUHUSU MAMBO YA KUZINGATIA WAKATI WA KUFUNGUA SHAURI LA MADAI KAHAMA, SHINYANGA.
27 Oct 2026
TUME YA KUREKEBISHA...

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, kupitia Kitengo cha Elimu kwa Umma, imetoa elimu ya sheria kwa wananchi kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kufungua shauri la madai.

Elimu hiyo imetolewa leo tarehe 26.10.2026 kupitia kituo cha redio cha Gold FM kilichopo Manispaa ya Kahama, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Tume za kuwajengea uelewa wananchi kuhusu sheria na utaratibu wa kufungua shauri la madai katika vyombo vya utoaji haki.

Katika elimu hiyo, iliyotolewa na Bw. Baraka Chipamba na Bi Latifa Mustapha ambao ni Mawakili wa Serikali kutoka Tume hiyo walisema sheria inawataka wananchi kuzingatia mambo mbalimbali kabla ya kufungua shauri la madai ikiwa ni pamoja na kutambua aina ya madai, chanzo au kiini cha mgogoro, mamlaka ya mahakama kisheria ya kusikiliza migogoro husika pamoja na kuzingatia ukomo wa muda uliowekwa kisheria.

Aidha, wananchi wamehimizwa kuzingatia muda wa kisheria wa kufungua mashauri ya madai, kwakuwa sheria imeanisha ukomo wa muda kwa mashauri mbalimbali ya madai. Kuzingatia masuala yaliyowekwa kisheria kabla ya kufungua mashauri ya madai ni muhimu ili kuepuka changamoto zinazoweza kuathiri haki ikiwemo kupoteza rasilimali fedha na muda wa kushughulikia madai ambayo hayakuzingatia sheria wakati wa kufungua katika vyombo husika.

Vilevile, imefafanuliwa umuhimu wa kuandaa nyaraka na vielelezo vinavyohusiana na madai, ikiwemo Hati ya Madai,Mkataba, Hati za Umiliki na ushahidi mwingine unaoweza kuthibitisha madai. Wananchi pia wanashauriwa kutafuta ushauri wa kisheria pale wanapohitaji ufafanuzi zaidi kuhusu taratibu za kufungua shauri.

Kupitia elimu hiyo,Tume imelenga kuwajengea wananchi uelewa wa msingi kuhusu haki na wajibu wao katika masuala ya madai, ili waweze kufanya maamuzi sahihi na kufuata taratibu zinazotakiwa kisheria wanapotafuta haki zao.

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inaendelea kutekeleza jukumu lake la kutoa elimu ya sheria kwa umma kwa kutumia njia mbalimbali za mawasiliano, ikiwemo vyombo vya habari, ili kuongeza uelewa wa maboresho mbalimbali ya sheria kwa wananchi.