MOROGORO. Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeshiriki Maonesho ya Biashara ya Moro Expo 2026 yanayofanyika katika Uwanja wa Stendi ya Zamani ya Daladala, mjini Morogoro, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu masuala mbalimbali ya sheria na mchango wake katika kukuza biashara na uwekezaji nchini.
Maonesho hayo yamehusisha jumla ya taasisi 26, ambapo taasisi 21 ni za ndani ya nchi na tano kutoka nje ya nchi, zikiwemo Kenya,Uganda, Rwanda, Burundi na Zambia.
Lengo la maonesho hayo ni kukuza biashara, uwekezaji na mitaji, pamoja na kuimarisha mitandao ya kibiashara baina ya wadau mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kupitia maonesho hayo, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeendelea kutoa elimu ya sheria kwa wananchi wa Mkoa wa Morogoro, kwa kuwafahamisha masuala mbalimbali ya kisheria yanayohusu maisha yao ya kila siku, biashara, mikataba na shughuli za kiuchumi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Meya wa Manispaa ya Morogoro, Mhe. Halidi Matengo, ambaye alikuwa mgeni rasmi, amewataka washiriki kutumia jukwaa hilo kutoa elimu ya sheria kwa wananchi ili waweze kuelewa mazingira wanayoishi na kufanya shughuli zao.
“Tutumie jukwaa hili kutoa elimu ya sheria kwa wananchi kuhusu mazingira yanayowazunguka, ikiwemo masuala ya mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali hapa nchini, ili wananchi waweze kuelewa haki na wajibu wao wanapoingia katika makubaliano ya mikopo,” amesema Mhe. Matengo.
Ushiriki wa Tume katika maonesho hayo ni sehemu ya mkakati wake wa kusogeza huduma za elimu ya sheria karibu na wananchi, kuwawezesha kutambua haki na wajibu wao na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa sheria bora na wezeshi katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, kupitia elimu hiyo, wananchi wanapata fursa ya kufahamu umuhimu wa kuzingatia sheria katika shughuli za biashara na uwekezaji, jambo linalosaidia kujenga mazingira bora ya kufanya biashara na kuchangia kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.