Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imeshiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, yanayoendelea kufanyika kuanzia leo tarehe 16 hadi 23 Juni 2026 katika viwanja vya Chinangali Park, Jijini Dodoma.
Maadhimisho hayo yamezikutanisha taasisi mbalimbali za Serikali na wananchi ambapo mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu”, ikiwa ni msisitizo wa kuimarisha uwazi, uwajibikaji na ubora wa huduma za umma nchini.
Aidha katika mpango wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania umebainisha kwamba itatumia jukwaa hilo muhimu kuelimisha umma kuhusu majukumu yake ya msingi ya Mapitio, Tathmini, na Utafiti juu ya maboresho ya sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili ziendane na mahitaji ya sasa ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia.
Hata hivyo TUME, itatumia Wiki ya Utumishi wa Umma kama fursa muhimu ya kusikiliza maoni ya wananchi, hasa kuhusu changamoto za kisheria zinazowakabili katika maisha yao.
Aidha Serikali imeendelea kusisitiza kuwa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ni nyenzo muhimu ya kuimarisha uwajibikaji na kuboresha utoaji wa huduma, huku ikihimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili kunufaika na huduma zitakazotolewa.
Maadhimisho ya mwaka huu yanatarajiwa kuhitimishwa rasmi tarehe 23 Juni 2026, ambapo viongozi wa serikali watahimiza utekelezaji wa maazimio yatakayolenga kuboresha utumishi wa umma na huduma kwa wananchi.