Naibu Katibu Mtendaji Tume ya Kurekebisha sheria Tanzania Bw. Burhan Kishenyi, leo tarehe 30.07.2026 amefungua warsha ya uelimishaji kuhusu Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, Sura ya 183, inayolenga kuimarisha uelewa wa wadau katika kuhakikisha sheria hiyo inatekelezwa kwa ufanisi sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Warsha hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, jijini Dodoma, na imewakutanisha washiriki kutoka taasisi mbalimbali za umma na wadau wanaoshughulika na masuala ya haki na ustawi wa watu wenye ulemavu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Bw. Kishenyi amesema kuwa utekelezaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ni msingi muhimu katika kujenga jamii jumuishi inayotoa fursa sawa kwa wananchi wote bila ubaguzi.
Amesisitiza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaweka msisitizo katika ushirikishwaji wa makundi yote ya jamii, ikiwemo watu wenye ulemavu, ili kuchangia kikamilifu maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha, amewataka washiriki kutumia warsha hiyo kujadili kwa kina wajibu wa kila taasisi katika kutekeleza matakwa ya sheria, kubadilishana uzoefu na kuibua mapendekezo yatakayosaidia kuondoa vikwazo vinavyokwamisha upatikanaji wa haki na huduma kwa watu wenye ulemavu.
Washiriki wa warsha hiyo wanatarajiwa kujengewa uwezo kuhusu tafsiri na utekelezaji wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu, pamoja na namna ya kuoanisha utekelezaji wake na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inalenga kujenga Tanzania jumuishi, yenye usawa, haki na maendeleo endelevu kwa wananchi wote.
Kwa upande wake , Bw. Harold Sungusia, Rais Mstaafu wa TLS ambaye pia ni wakili wa kujitegemea alisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika mchakato wa maboresho ya sheria ili kuhakikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inatekelezwa kwa misingi ya usawa, haki na ushirikishwaji.
Akizungumza katika mkutano uliojadili mwelekeo wa maboresho ya sheria na maendeleo ya taifa, Bw. Sungusia alisema kuwa sheria bora zinapaswa kuzingatia mahitaji ya makundi yote ya jamii, ikiwemo watu wenye ulemavu, ili wasibaki nyuma katika safari ya maendeleo.
Alieleza kuwa ushiriki wa watu wenye ulemavu katika utoaji wa maoni na maamuzi kuhusu sheria ni muhimu kwa sababu unasaidia kutunga na kuboresha sheria zinazolinda haki zao na kuondoa vikwazo vinavyowazuia kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Aidha, alibainisha kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji mfumo wa sheria unaohakikisha fursa sawa kwa wananchi wote bila ubaguzi wa aina yoyote.
Bw. Sungusia alisema kuwa kujenga taifa lenye maendeleo endelevu kunategemea uwepo wa sheria jumuishi zinazolinda haki za kila mwananchi na kuweka mazingira yanayowawezesha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Washiriki wa mkutano huo walikubaliana kuwa ushirikishwaji wa makundi maalumu katika mchakato wa maboresho ya sheria ni nguzo muhimu ya kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kujenga jamii yenye usawa na haki kwa wote.