Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amezindua rasmi Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, huku akitoa wito kwa watumishi wa umma kuendelea kuimarisha uwajibikaji, ubunifu na matumizi ya teknolojia za kidijitali katika utoaji wa huduma kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Kikwete alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kufanya maboresho makubwa katika sekta ya utumishi wa umma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, za haraka na zenye kuzingatia maadili ya kazi za umma.
Alisema maadhimisho hayo ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha wananchi na taasisi za umma, ambapo wananchi wanapata fursa ya kupata huduma mbalimbali papo kwa papo pamoja na kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha utoaji wa huduma serikalini.
“Mageuzi ya kidijitali yanapaswa kuwa sehemu ya utamaduni wetu wa kazi. Tunapaswa kutumia mifumo ya kisasa kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika kuwahudumia wananchi,” alisema Mhe. Kikwete.
Aidha, aliwataka watumishi wa umma kuendelea kuzingatia misingi ya uadilifu, uzalendo na kuwahudumia wananchi kwa weledi, akisisitiza kuwa maendeleo ya Taifa yanategemea ubora wa huduma zinazotolewa na taasisi za umma.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Juma Selemani Mkomi alisema maadhimisho hayo yanahusisha ushiriki waTaasisi 225 ikilinganishwa na 146 ya mwaka jana zikihusisha wizara, taasisi za umma wakala wa serikali na wadau mbalimbali ambao wanatoa elimu na huduma kwa wananchi kwa kipindi chote cha wiki hiyo huku akizipongeza taasisi hizo kwa ushiriki wao.
Aidha Mhe.Waziri ameelekeza Taasisi na wizara zote kuendelea kuenda kushiriki katika majukwaa mbalimbali kwa ajili ya kuhudumia wananchi na kuyatangaza mambo mema yanayofanywa na Serikali.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni na hufikia kilele chake katika Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika, inayoadhimishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika.
Wananchi wa Dodoma na maeneo jirani wameendelea kujitokeza kwa wingi kutembelea mabanda mbalimbali ya maonesho ili kupata huduma, elimu na ufafanuzi kuhusu shughuli zinazotekelezwa na taasisi za umma nchini.