Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

PROF. IBRAHIMU JUMA: TUME YA KUREKEBISHA SHERIA  IPIME UFANISI WA SHERIA  KWA VITENDO.
01 Sep 2026
PROF. IBRAHIMU JUMA:...

Jaji Mkuu mstaafu Prof. Ibrahimu Juma ameishauri Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kutafuta mbinu bora ya kubaini namna sheria zinavyofanya kazi kwa vitendo, ili maboresho yanayofanyika yaweze kuendana na changamoto halisi za jamii katika kipindi cha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Prof. Juma ametoa ushauri huo tarehe 1 Septemba , 2026 katika ukumbi wa Hoteli ya Girwill jijini Dodoma, akisisitiza kuwa uwepo wa sheria pekee hautoshi kuhakikisha wananchi wanazifuata na kwamba kinachohitajika ni kutathmini kwa kina utekelezaji wake katika mazingira halisi.

Ametoa mfano wa masuala ya masoko, ujenzi holela na utupaji taka kiholela, akisema licha ya kuwepo kwa sheria na kanuni zinazodhibiti maeneo hayo, bado ukiukwaji wake unaendelea kwa kiwango kikubwa.

Kwa mujibu wa Prof. Juma, hali hiyo inapaswa kuifanya Tume ya Kurekebisha Sheria kuangalia zaidi ya kutunga au kurekebisha sheria, bali pia kuchunguza sababu zinazowafanya wananchi kushindwa au kutotaka kuzifuata.

Amesema ni muhimu sheria zinazofanyiwa marekebisho zielekezwe pia katika kushughulikia tabia na mazingira yanayochochea ukiukwaji wa sheria, badala ya kutegemea adhabu pekee baada ya sheria kukiukwa.

“Ni muhimu kujua sheria inafanya kazi vipi katika mazingira halisi. Kama sheria ipo lakini ukiukwaji unaendelea, lazima tujiulize ni kwa nini watu hawafuati sheria hiyo na ni nini kinachoweza kufanyika kubadili hali hiyo,” amesisitiza.

Amesema mtazamo huo utasaidia kujenga mfumo wa sheria unaozingatia uhalisia wa maisha ya wananchi na kutoa majibu kwa changamoto zinazojitokeza katika jamii.

Ushauri huo unakuja wakati ambapo Serikali inaendelea kuweka mkazo katika maboresho ya mfumo wa sheria ili kuendana na mahitaji ya sasa na ya baadaye katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. 


Awali akitoa neno la ukaribisho Katibu Mtendaji Tume ya Kurekebisha sheria Tanzania  Bw. George Mandepo, alieleza kuwa miongoni mwa majukumu Tume  ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa sheria na kupendekeza maboresho yanayozifanya ziendane na mazingira ya Tanzania.

Aidha,  Bw. Mandepo alisisitiza umuhimu wa maboresho ya sheria katika kuwezesha utekelezaji wa Dira 2050, na kufanya tafiti na mapitio katika maeneo mbalimbali ya kisheria.

Prof. Juma amesisitiza kuwa katika safari ya kuelekea Tanzania ya 2050, mafanikio ya sheria hayapaswi kupimwa kwa kuangalia tu kama sheria imetungwa, bali pia kwa kuangalia matokeo yake katika maisha ya kila siku ya wananchi.