Wazee wa mabaraza ya kata mkoani Tanga wamesema kuwa migogoro inayohusu ardhi, ndoa, mirathi pamoja na malezi ya watoto imeendelea kuwa changamoto kubwa inayowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali ya mkoani Tanga.
Wakichangia katika kipindi cha maswali na majibu mara baada ya kupatiwa elimu ya sheria kuhusu uendeshaji wa mabaraza ya kata kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Mkuu wa mkoa huo, wazee hao walieleza kuwa wanapokea mashauri mengi kila siku, huku migogoro ya ardhi ikiongoza kwa wingi kutokana na ongezeko la thamani ya ardhi na ukosefu wa mipaka sahihi katika baadhi ya maeneo.
“Masuala ya ardhi yamekuwa yakileta mvutano mkubwa kati ya familia na hata majirani, hasa pale mipaka inapokuwa haijawekwa wazi au kumiliki kisheria,” alisema mmoja wa wazee wa baraza hilo.
Mbali na hilo, walibainisha kuwa migogoro ya ndoa imekuwa ikiongezeka, ikihusisha kutokuelewana kati ya wanandoa, migogoro ya kifedha na ukatili wa majumbani. Walisema hali hiyo imekuwa ikiathiri ustawi wa familia na maendeleo ya watoto.
Aidha, wazee hao walitaja migogoro ya mirathi kuwa ni chanzo kingine kikubwa cha migawanyiko ndani ya familia, hususan pale ndugu wanaposhindwa kufikia muafaka kuhusu ugawaji wa mali za marehemu.
Kuhusu malezi ya watoto, walieleza kuwa wazazi wengi wanakabiliwa na changamoto za malezi bora, hali inayochangia baadhi ya watoto kujingiza katika vitendo vya uhalifu na mmomonyoko wa maadili.
Wazee hao walitoa rai kwa wananchi kuzingatia sheria na taratibu, pamoja na kutafuta suluhu ya migogoro kwa njia ya mazungumzo na usuluhishi kabla ya kufikia hatua za kisheria.
Pia waliitaka serikali na wadau mbalimbali kuongeza juhudi katika utoaji wa elimu kuhusu haki za ardhi, masuala ya ndoa, mirathi na malezi bora ya watoto ili kupunguza migogoro hiyo katika jamii.