Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

MABORESHO YA SHERIA NI MUHIMU KATIKA KUFIKIA MALENGO YA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050
19 Jun 2026
MABORESHO YA SHERIA...

 

Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRTC), Bw. George Mandepo, ametoa wito kwa watumishi wa Tume hiyo kuendelea kufanya maboresho ya kisheria yatakayoiwezesha Tanzania kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na mifumo ya sheria inayoweza kujibu changamoto za sasa na za baadaye.

Bw. Mandepo amesema kuwa sheria za nchi zinapaswa kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya sayansi, teknolojia, biashara na uwekezaji ili kuchochea ubunifu, kuongeza ushindani wa kiuchumi na kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.

Katibu Mtendaji huyo alitoa kauli hiyo leo, tarehe 18 Juni 2026, wakati akifungua kikao kazi cha mafunzo kuhusu mfumo wa sheria zinazosimamia masuala ya nishati pamoja na mfumo wa sheria za viwanda, biashara na uwekezaji kilichofanyika katika Hoteli ya APC Bunju, jijini Dar es Salaam.

"Tunapoelekea Tanzania ya mwaka 2050, ni muhimu kuwa na mifumo ya sheria inayoweza kujibu changamoto za sasa na za baadaye. Sheria hizo zinapaswa kuchochea ubunifu, kuimarisha ushindani wa kiuchumi, kuendeleza matumizi ya teknolojia na kuvutia uwekezaji wenye tija kwa maendeleo ya taifa," alisema Bw. Mandepo.

Alieleza kuwa mabadiliko yanayotokea katika mazingira ya biashara, uwekezaji na maendeleo ya teknolojia duniani yanahitaji tathmini na maboresho ya mara kwa mara ya mifumo ya sheria ili kuhakikisha inaendelea kuwa rafiki kwa maendeleo ya taifa na mahitaji ya wananchi.

Kwa mujibu wa Bw. Mandepo, sekta za nishati, viwanda, biashara na uwekezaji ni nguzo muhimu za uchumi wa taifa, hivyo zinahitaji kuongozwa na sheria zinazoweka mazingira bora ya ukuaji, ushindani na uwekezaji katika soko la kikanda na kimataifa.

Aidha, alisema kuwa sheria zilizoboreshwa zitakuwa na matokeo chanya ikiwemo kuongeza tija na ufanisi wa taasisi za umma kwa kupunguza urasimu usio wa lazima, kuimarisha uwajibikaji na kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wananchi. Aliongeza kuwa uwepo wa sheria madhubuti na za kisasa utavutia mitaji ya ndani na nje ya nchi na hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda na uchumi wa kidijitali.

Bw. Mandepo alibainisha kuwa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania tayari imejipanga kushirikiana kwa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, Wizara, Taasisi za Umma, Sekta Binafsi na wadau mbalimbali katika kufanya mapitio ya sheria zinazohusiana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Alisema ushirikiano huo utalenga kufanya uchambuzi wa kina wa sheria zilizopo, kubaini maeneo yenye vikwazo kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na kupendekeza maboresho yatakayowezesha uwekezaji, matumizi ya teknolojia za kisasa, maendeleo ya viwanda, biashara na utoaji bora wa huduma kwa wananchi.

"Tume imejipanga kuhakikisha kuwa mchakato wa maboresho ya sheria unakuwa shirikishi, jumuishi na unaozingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye ya taifa. Kupitia ushirikiano na taasisi husika, tutafanya mapitio ya sheria na mifumo ya udhibiti ili kuhakikisha inaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," alisema.

Aliongeza kuwa Tume itaendelea kufanya tafiti, kupokea maoni ya wadau na kufanya tathmini za athari za sheria na kanuni mbalimbali ili kuhakikisha mapendekezo yatakayotolewa yanajibu changamoto halisi za maendeleo na kuongeza ushindani wa Tanzania katika uchumi wa kikanda na kimataifa.

Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka EWURA, Dk. Suleiman Serera, amesema kuwa Tanzania ina wajibu wa kuendelea kuboresha baadhi ya sheria zake ili ziwe kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hususan katika kipindi hiki ambacho taifa linaanza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Dk. Serera alisema kuwa sheria zina nafasi muhimu katika kuunda mazingira bora ya uwekezaji, ubunifu, biashara na utoaji wa huduma kwa wananchi, hivyo zinapaswa kwenda sambamba na mahitaji ya wakati.

"Tuna kazi ya kuendelea kuboresha sheria zetu ili ziweze kuwa kichocheo cha maendeleo, hasa katika kipindi hiki tunapotekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050," alisema.

Alieleza kuwa mabadiliko ya teknolojia, ukuaji wa sekta binafsi na ushindani wa kimataifa vinahitaji mfumo wa sheria unaoendana na hali halisi ya sasa na matarajio ya baadaye ya taifa.

Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kufanya mapitio ya sheria, kanuni na taratibu mbalimbali ili kuhakikisha zinasaidia ukuaji wa sekta za uzalishaji, teknolojia, viwanda, kilimo na biashara.

Nae Wakili Prudence Rweyongeza kutoka Ofisi ya Rais, Uwekezaji, ametoa mada ya changamoto za kisheria zinazopaswa kuzingatiwa kwenye Maboresho yatalayofanyika ili kuvutia wawekezaji. Ameeleza pamoja na masuala mengine, ni muhimu kutazama kwa umakini vivutio vya uwekezaji, mifumo ya utatuzi wa migogoro, urahishaji wa utoaji wa vibali, leseni za biashara na mifumo ya usimamizi. Aidha, amesisitiza kutazama kwa kina utendaji wa taasisi muhimu ili kuweka mifumo ya kisheria wa kuboresha huduma. 

Kikao kazi hicho kimewakutanisha wataalamu na wadau kutoka Tume hiyo pamoja na taasisi mbalimbali zinazohusika na maboresho ya sheria zinazogusa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa lengo la kujadili na kuongeza uelewa kuhusu mifumo ya sheria inayosimamia masuala ya nishati, viwanda, biashara na uwekezaji.

Kikao hicho ni moja ya hatua muhimu za kujenga uwezo wa mawakili wa Serikali na wataalamu watakaoshiriki katika mchakato wa mapitio na maboresho ya mifumo ya kisheria. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuimarisha uwezo wa kitaasisi katika kubuni na kusimamia sheria zinazochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini na kusaidia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.