Katibu Mtendaji wa Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania Bw. George Mandepo amesema Tume hiyo imejipanga vyema katika kufanya Maboresho ya Sheria nchini ili kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Bw. Mandepo ameyasema hayo Julai 2, 2026 wakati akizungumza na waandishi wa Habari wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea Jijini Dar es salaam.
Katika hatua hiyo Bw.Mandepo amegusia kuwa mpaka sasa Tume hiyo imeshaanza mchakato wa maboresho ya mfumo wa Sheria kupitia tafiti mbalimbali ikiwa ni pamoja na utafiti wa Sheria kuhusiana na masuala ya Nishati, Sheria kuhusiana na masuala ya Uwekezaji, na Sheria zinazohosu masuala ya Viwanda na Biashara.
“Katika kipindi hiki miongoni mwa mambo makubwa ambayo tume inatekeleza ni kufanya Maboresho ya sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili ziweze kuendana na malengo ya Dira ya Taifa ya maendeleo 2050”. Alisema Mandepo
Pia alieleza kuhusu utafiti wa mfumo wa Sheria zinazosimamia mambo ya Kidijitali kama vile Biashara ya Uchumi wa kimtandao pamoja na Utafiti kuhusu mfumo wa Sheria zinazosimamia Biashara ya Kaboni (Hewa Ukaa).
Kwa upande wake Naibu katibu ambaye ni Mkuu wa kitengo cha elimu ya sheria kwa umma, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bi. Zainab chanzi alisema Dira ina misingi, ina vichocheo na sekta za kimageuzi na kubainisha kuwa sheria ndio chombo muhimu katika kuhakikisha malengo ya Dira hiyo yanafikiwa.
Bi. Zainab aliendelea kusema pamoja na mjukumu ya Tume hiyo katika kufanya maboresho ya sheria lakini imekua ikitekeleza wajibu wa kutoa elimu ya Sheria katika jamii kwakua elimu wanayojengewa wananchi inaaonyesha fursa zilizopo, wajibu na haki zao ambazo zinakua zimetolewa katika sheria mbalimbali.
“Elimu tunayowajengea wananchi inawaonyesha fursa zilizopo, tunawaonyesha wajibu na haki zao zilizoainishwa katika sheria mbalimbali” alisema Bi. Zainab
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inashiriki maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) 2026 kwa lengo la kutoa eliku ya sheria kwa umma na kupokea maoni ya kuhusu maboresho ya sheria mbalimbali.