Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imetoa elimu ya sheria kuhusu uendeshaji na umuhimu wa mabaraza ya Kata katika utatuzi wa migogoro ya wananchi wa mkoani Tanga,
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Bw. Baraka Chipamba wakili kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania alisema lengo kuu ni kuwawezesha wananchi kuelewa majukumu ya mabaraza ya kata, namna ya kuyatumia katika kutatua migogoro ikiwemo ya Ardhi pamoja na haki na wajibu wao kisheria.
Bw. Chipamba alieleza kwamba wananchi wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu nafasi ya mabaraza ya kata katika mfumo wa haki, hali inayosababisha baadhi yao kukimbilia mahakamani hata kwa migogoro midogo ambayo ingeweza kutatuliwa kwa njia ya usuluhishi.
“Tunatoa elimu hii ili wajumbe na wananchi watambue kuwa mabaraza ya kata ni chombo muhimu cha kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi kwa haraka, kwa gharama nafuu na kwa kuzingatia maridhiano ili jamii iwe yenye utulivu na amani” alisema.
Aidha, Baraka alibainisha kuwa elimu hiyo inalenga pia kuwajengea uwezo wajumbe wa mabaraza ya kata ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo.
Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema itawasaidia kushughulikia migogoro ya jamii kwa ufanisi zaidi.
Aidha wajumbe wa mabaraza ya kata walieleza kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka, hasa katika kipindi ambacho migogoro ya ardhi na ndoa imekuwa ikiongezeka katika jamii.
Tume hiyo imeahidi kuendelea kutoa elimu katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata uelewa wa masuala ya kisheria na kutumia ipasavyo vyombo vya utatuzi wa migogoro vilivyopo katika ngazi ya jamii.