Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

LRCT WAHIMIZWA KUTAZAMA SHERIA KUHUSU MALIPO YA FEDHA KIDIJITALI .
01 Jul 2026
LRCT WAHIMIZWA KUTAZ...

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Zainab Katimba ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Kufanya Maboresho ya Sheria za Kidijitali (Digital Laws) ili kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.

Mhe. Katimba aliyasema hayo leo Julai 1, 2026 alipotembelea Banda la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara, yanayoendelea katika Viwanja vya SabaSaba Jijini Dar Es Salaam.

Mhe. Katimba alisema Tume ya kurekebisha Sheria, imebeba dhima kubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kwamba mpango huo hautaweza kufanikiwa ikiwa hakutakua na sheria wezeshi, Sheria ambazo zitatoa fursa kwa Taasisi mbalimbali kutimiza majukumu yake pamoja na ujumla wa utekelezaji wa Dira 2050.

"Taasisi hii imebeba dhima kubwa sababu utekelezaji wa Dira 2050 hauwezi kufanikiwa kama hakuna Sheria wezeshi" alisema Mhe. Katimba

Katika hatua hiyo Naibu Waziri alisema anafahamu hatua ambazo Tume imefikia katika kufanya Mapitio ya Sheria mbalimbali ili kuwezesha utekelezaji wa malengo yaliowekwa kwenye Dira 2050 na kusisitiza sheria zinazogusa masuala ya malipo ya fedha kidijitali zitazamwe kutokana na kasi ya mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.

Aidha alisisitiza kutazama Maboresho ya Sheria kuhusu Matumizi ya Akili Unde (AI) kutokana na kuwepo kwa wimbi kubwa la watumiaji wa teknolojia hiyo ili kudhibiti matumizi yasio sahihi kwa ustawi wa maendeleo ya Taifa.

Awali Afisa Sheria wa Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania Baraka Chipamba alimueleza Naibu waziri huyo kuwa Tume ipo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) kwa lengo la kutoa elimu ya sheria na kupokea maoni kuhusu mapendekezo ya maboresho ya sheria mbalimbali kwa wananchi na kwamba maboresho hayo yatawezesha utekelezaji wa mipango wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

"Pamoja na majukumu yetu ya kufanya Mapitio na Utafiti wa Sheria mbalimbali lakini tupo hapa kwa lengo la kutoa elimu ya sheria na kupokea maoni kwa wananchi kuhusu mapendekezo ya maboresho ya sheria mbalimbali ili kuendana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii" alisema Baraka

Tume inashiriki Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara yalioanza Juni 28 na kutegemewa kuhitimishwa Julai 13, 2026 ili kukusanya maoni na kutoa elimu ya Sheria kwa Wananchi.