Bagamoyo
Mwanasheria Vicky Mbunde kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT), amesema kuandika wosia siyo uchuro bali unasaidia kuondoa migogoro ya kugombea mali zilizoachwa na marehemu.
Hayo yalibainishwa na mwanasheria huyo Aprili 25, 2025 wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Magomeni mjini Bagamoyo Mkoa wa Pwani wakati akitoa elimu inayohusu umuhimu wa kuandika Wosia pamoja na kujiepusha na makosa mbalimbali ya kimtandao.
Alisema makosa ya kimtandao yamekuwa yakifanyika kwa kutumia vifaa vya kielektroniki kama kompyuta, simu janja, vishikwambi na Teknolojia ya Mawasiliano ya Habari (TEHAMA).
Mbunde alisema wosia ni nyaraka ya kisheria ambayo inaonyesha matakwa na maagizo ya mtu kuhusu namna mali yake itakavyogawiwa baada ya kifo chake na kuwa unaweza kujumuisha maelekezo kuhusu jinsi mali itakavyogawiwa kwa warithi, uteuzi wa wasimamizi wa mali, na mambo mengine yanayohusiana na urithi wa mtu husika.
" Malengo ya kuandika wosia ni kuhakikisha kwamba matakwa ya mtu yatatekelezwa ipasavyo baada ya kifo chake na kuwa unaweza kuwa na athari za kisheria na unaweza kutambulika na mahakama mara tu baada ya kifo cha mtu aliyeandika wosia huo," alisema Mbunde.
Mbunde alisema wosia unaweza kujumuisha mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na uteuzi wa warithi na kuonyesha ni nani atakayepokea mali za marehemu.
Alisema mtu anaweza kuteua watu wa kusimamia mali zake na kutekeleza matakwa yake kama watekelezaji wa wosia ambao unaweza kuainisha jinsi mali inavyopaswa kutumika, kugaanywa, au kuhamishwa kifedha.
Alisema kama marehemu aliacha wosia na kumchachagua mtu wa kusimamia na kugawa mirathi yake baada ya yeye kufariki, ataomba mahakamani kuthibitisha wosia huo.
Aliongeza kuwa kama hakuna wosia, hatua ya kwanza ni kuchagua msimamizi wa mirathi. ambaye ndugu wa marehemu watalipendekeza jina lake ili asimamie mirathi.
Alisema kazi ya msimamizi wa mirathi ni kufungua Mahakamani shauri la maombi ya kusimamia mirathi, kubainisha, kukusanya na kuhifadhi mali za marehemu, kulipa madeni yaliyoachwa na marehemu na kugawa kilichobaki kwa warithi halali.
Chipamba alisema siyo kila mahakama inaweza kusikiliza kesi hizo za mirathi ambapo amezitaja mahakama ambazozinasikiliza mashauri hayo kuwa ni Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya. Mahakama ya Hakimu Mteule na Mahakama Kuu.
Alisema unaweza kwenda Mahakama ya Mwanzo kama mirathi inahusisha sheria za Kimila au za Kiislam na hiyo haijalishi thamani na ukubwa wa mirathi husika hivyo kama wewe ni Mkristo, usiende Mahakama ya Mwanzo na utaenda Mahakama ya Mwanzo iwapo sheria inayotumika kwenye hiyo mirathi ni ya Kimila au Kiislam.
Aidha Chipamba alisema Mahakama ya Wilaya inasikiliza mashauri ya mirathi ambayo haizidi Sh.100,000,000 kwa hiyo chochote chenye thamani ya kuanzia sifuri mpaka million mia ni shauri dogo ambalo litasikilizwa.
" Usiende Mahakama ya Mwanzo, hata kama mirathi ni fedha ndogo. Utatakiwa kwenda Mahakama ya iwapo tu sheria inayotumika ni ya kimila au kiislam," alisema Chipamba.