Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe.Winifrida Korosso, leo tarehe 16.09. 2025 ameongoza kikao maalum na watumishi wa Tume hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi za Tume zilizopo katika majengo ya chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Lengo la kikao hicho kilikuwa ni kujadili mambo mbalimbali yanayohusu ufanisi wa Tume, mazingira ya kazi, pamoja na kuhimiza mshikamano na uwajibikaji miongoni mwa watumishi.
Katika hotuba yake, Jaji Korosso aliwataka watumishi wa Tume kuendelea kuwa na moyo wa kujituma, kufanya kazi kwa weledi na kushirikiana kwa karibu ili kutimiza majukumu ya Tume kwa ufanisi.
Alisisitiza kuwa kazi ya kurekebisha sheria ni ya msingi sana kwa maendeleo ya taifa na inahitaji umakini mkubwa, maarifa na maadili ya hali ya juu.
Aidha Mwenyekiti huyo alitumia muda huo kutoa pongezi kwa washiriki wa michezo ya shimiwi ambapo aliwataka kuendelea kufanya mazoezi ili kuimarisha timu hiyo badala ya kusubiri mpaka mwakani wakati wa michezo hiyo.
“Tunalo jukumu kubwa la kuhakikisha sheria zetu zinaendana na mahitaji ya sasa ya jamii ya Kitanzania. Hili linahitaji ushirikiano wa karibu baina yetu sote kama watumishi wa umma,” alisema Jaji Korosso.
Aidha, kikao hicho kilitoa fursa kwa watumishi kutoa maoni, mapendekezo na kuwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Masuala kama uboreshaji wa mazingira ya kazi, matumizi ya TEHAMA, na upatikanaji wa rasilimali stahiki yalijadiliwa kwa kina.
Mwenyekiti aliahidi kuyafanyia kazi maoni na mapendekezo yaliyotolewa, na kusisitiza kuwa uongozi wa Tume utaendelea kuwa karibu na watumishi wote katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira bora ya kufanikisha majukumu ya taasisi hiyo.
Kikao hicho kimetajwa kuwa sehemu ya mikakati ya Tume katika kujenga utamaduni wa mawasiliano ya wazi na kuimarisha ufanisi katika utendaji kazi wa kila siku.