Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

MAFUNZO YA USIMAMIZI WA VIHATARISHI YAONGEZA UFANISI KWA WATUMISHI WA TUME YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA
15 Dec 2025
MAFUNZO YA USIMAMIZI...

Watumishi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania wamenufaika na mafunzo ya usimamizi wa vihatarishi (Risk Management) yaliyofanyika leo tarehe 15/12/2025 katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Parrot, iliyopo mjini Arusha, kwa lengo la kuwawezesha kutambua, kuchambua na kudhibiti vihatarishi vinavyoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Tume hiyo.
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea washiriki uelewa wa kina kuhusu dhana ya usimamizi wa vihatarishi, umuhimu wake katika taasisi za umma, pamoja na mbinu bora za kutambua na kupima vihatarishi katika utekelezaji wa kazi za kila siku, hususan katika mchakato wa urekebishaji wa sheria nchini.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mtendaji, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi, Bw. Mohamed Mavura alisema kuwa usimamizi madhubuti wa vihatarishi ni nguzo muhimu katika kuimarisha utawala bora, uwajibikaji na ufanisi wa taasisi, akisisitiza kuwa Tume inapaswa kuwa tayari kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria.
Bw. Mavura alieleza kwamba mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania katika kujenga uwezo wa watumishi wake, kuboresha mifumo ya usimamizi na kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya Tume unazingatia viwango vya kitaifa na kimataifa vya utawala bora.
Kwa upande wake Bw. Alphonce Muro Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa ndani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya makazi alieleza kwa kina dhana ya usimamizi wa vihatarishi, aina mbalimbali za vihatarishi vinavyoweza kujitokeza katika taasisi za kisheria, pamoja na mbinu bora za kuvitambua, kuvichambua na kuvithibiti ili kupunguza athari zake katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Aidha, Bw. Alphonce aliwahimiza watumishi wa Tume kuzingatia usimamizi wa vihatarishi kama sehemu ya utamaduni wa kazi, akisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kuboresha upangaji wa kazi, kufanya maamuzi sahihi na kufanikisha malengo ya taasisi kwa wakati.
Katika mafunzo hayo, washiriki walijifunza masuala mbalimbali yakiwemo utambuzi wa vihatarishi vya kimkakati, kiutendaji, kisheria na kiusimamizi, namna ya kuandaa Risk Register, pamoja na kuweka mikakati ya kudhibiti vihatarishi ili kupunguza athari zake kwa Tume.

Washiriki wa mafunzo hayo walieleza kuridhishwa na maudhui yaliyotolewa, wakisema yamewaongezea ujuzi na maarifa yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi na kwa kuzingatia kanuni za usimamizi bora wa vihatarishi.