Timu ya Wanawake Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (Tumesheria Sports Club) wamefanikiwa kuingia katika hatua ya timu 16 bora za mashindano ya kuvuta kamba Wanawake katika michuano ya SHIMIWI 2025, inayoendelea Jijini Mwanza.
Tumesheria wamefanikiwa kuingia hatua hiyo baada ya kumvuta mpinzani wake Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Pwani (Ras Pwani) kwa awamu ya awali na kutoa sare awamu ya pili, katika mchezo wa mwisho kukamilisha hatua ya makundi uvutaji wa kamba uliofanyika leo tarehe 5 Sepetemba 2025 asubuhi katika uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza.
Matokeo hayo yameipa nafasi Tumesheria kusonga mbele hatua inayofuata ya 16 bora, licha ya kusadikika huenda kukaja kuwa na mchezo mwingine wa kumtafuta mshindi wa kwanza katika kundi E kutokana na Tume sheria kuendelea kufungana kwa alama na timu ya Bunge ambao nao walivuta kamba dhidi ya Uwekezaji na kufanikiwa kushinda awamu ya kwanza na kutoa sare awamu ya pili na kufanya Tumesheria na Bunge zote kufungana alama ijapokua ndio timu zilizofuzu hatua ya 16 bora katika kundi lake E.
Itakumbukwa timu ya Tume sheria katika kundi E ilifanikiwa kushinda michezo 2 kwa mivuto yote ikatoa sare dhidi ya Bunge na ikashinda awamu ya kwanza na kutoa sare awamu ya pili dhidi ya Ras Pwani, na timu ya Bunge pia ilishinda michezo 2 ikapata sare 1 dhidi ya Tumesheria na kushinda dhidi ya Uwekezaji awamu ya kwanza na awamu ya pili kupata sare, na hiyo ndio sababu ya kufungana kwa alama kwa timu hizo mbili ambazo zote zimefuzu hatua ya 16 bora.
Ikiwa inasubiriwa ratiba ya mwendelezo wa michuano hiyo, Kwa mujibu wa uongozi wa SHIMIWI licha ya kuwa mashindano hayo yalishaanza tokea tarehe 1 Septemba 2025, imeelezwa kuwa ufunguzi rasmi wa michuano hiyo unategemewa kufanyika tarehe 7 Septemba 2025 katika uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.