Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania imekutana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar katika kikao kazi kilicholenga kuimarisha utekelezaji wa mkataba wa makubaliano ya ushirikiano (MoU) kati ya pande hizo mbili, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano katika mapitio, maboresho, na utafiti wa sheria zinazotekelezwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Kikao hicho kilichofanyika Zanzibar na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania pamoja na maafisa waandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar kilijadili mafanikio yaliyopatikana tangu kutiwa saini kwa makubaliano hayo, pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele ya kisheria kwa kipindi kijacho.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzani George Mandepo, alisema kuwa ushirikiano kati ya Tume na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar ni muhimu katika kuimarisha mfumo wa sheria nchini kwa kuzingatia mahitaji ya pande zote mbili za Muungano.
“Kupitia mkataba huu wa makubaliano, tunajenga msingi madhubuti wa kushirikiana katika kufanya tafiti za kisheria, kubadilishana uzoefu, na kuimarisha uwezo wa wataalamu wetu wa sheria kutoka pande zote mbili,” alisema.
Aidha Bw. Mandepo alisema kwamba LRCT kwa mwaka wa fedha 2025/26 imejipanga kufanya tafiti mbalimbali ikiwemo utafiti wa mfumo wa sheria zinazosimamia upingaji wa maamuzi ya kiutawala mahakamani,utafiti wa mfumo wa sheria zinazosimamia usajili wa Mawakili Tanzania na utafiti wa mfumo wa sheria unaosimamia biashara ya hewa ukaa.
Bw. Mandepo amefafanua kwamba Tume kwa sasa inaendelea kufanya mapitio ya sheria ya Bima sura ya 169, mapitio ya sheria ya Bima sura ya 394 na mapitio katika sheria ya afya na usalama mahala pa kazi Sura ya 297.
Hata hivyo alieleza kwamba Tume inafanya tathmini ya utekelezaji wa sheria za mamlaka ya nchi kuhusu umilikimali na maliasili za nchi sura ya 449 pamoja na sheria ya mapitio na majadiliano kuhusu masharti hasi katika mkataba wa mali asili na maliasilia sura ya 450.
Eneo lingine ambalo limetajwa kufanyiwa tahmini ni katika utekelezaji wa sheria ya ugaidi sura ya 19 sambamba na utoaji wa elimu ya sheria kwa Umma na uandaaji wa machapisho pamoja na ushiriki wa maonesho mbalimbali hapa nchini alimalizia Katibu Mtendaji.
Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Bw. Shaaban Abdalla, alieleza kuwa ushirikiano huo unaongeza tija katika kazi za uhuishaji wa sheria kwa kuhakikisha kwamba mabadiliko ya kisheria yanayoletwa yanazingatia uhalisia wa jamii zote.
“Tunaamini kuwa kazi za mapitio ya sheria zinahitaji ushirikiano wa karibu kati ya taasisi zote za kisheria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ushirikiano huu utasaidia pia kuondoa migongano ya kisheria na kujenga msingi wa sheria zinazotekelezeka kwa haki na usawa,” alisema.
Katika kikao hicho, wajumbe walikubaliana pia kuunda kikosi kazi cha pamoja kitakachoratibu utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele yaliyobainishwa katika MoU, ikiwemo masuala ya sheria za teknolojia, haki za binadamu, usuluhishi wa migogoro, na sheria za kimataifa zinazogusa pande zote za Muungano.
MoU kati ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar ilisainiwa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu, kubadilishana taarifa, na kujengeana uwezo katika nyanja mbalimbali za kisheria, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha maendeleo ya sheria yanaenda sambamba na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia.
MWISHO