Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

KAHAMA WANUFAIKA NA ELIMU YA SHERIA KUHUSU TARATIBU ZA UKAMATAJI NA HAKI ZA MTUHUMIWA
29 Oct 2026
KAHAMA WANUFAIKA NA...

KAHAMA, SHINYANGA,  
Mawakili wa Serikali kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Bi. Vicky Mbunde na Bw. Richard Mdee, leo tarehe 27.10.2026 wametoa elimu ya sheria kuhusu taratibu za ukamataji na haki za mtuhumiwa kupitia kituo cha redio cha KM 24 FM kilichopo katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.

Elimu hiyo imelenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa wakati wa kumkamata mtu pamoja na haki za msingi alizonazo mtuhumiwa kwa mujibu wa sheria.

Kupitia kipindi hicho, wananchi wa mkoa wa Shinyanga na mikoa ya karibu wamepata fursa ya kufahamu umuhimu wa kuzingatia sheria katika hatua za ukamataji, ili kuhakikisha kuwa taratibu zinazotumika zinazingatia haki, utu wa binadamu na misingi ya utawala wa sheria.

Aidha, walisema kwamba elimu hiyo inalenga kuwajengea wananchi  uelewa kuhusu haki  na wajibu wao pamoja na umuhimu wa kufahamu taratibu zinazotakiwa kufuatwa na vyombo vinavyohusika katika usimamizi na utekelezaji wa sheria.

"Elimu kwa umma kuhusu masuala mbalimbali ya haki jinai ni muhimu katika kuwawezesha wananchi kuelewa sheria na umuhimu wa kuzingatia katika maisha ya kila siku"  Walisema

Vilevile, Bi Vicky Mbunde alisema Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ina jukumu la kufanya mapitio ya sheria zote zilizotugwa na Bunge na kupendekeza maboresho ya sheria ili ziakisi mahitaji ya jamii na maendeleo ya nchi kwa wakati husika.                                                                                                              

  "Utoaji wa elimu ya sheria kupitia vyombo vya habari ni njia muhimu ya kufikisha elimu ya sheria kwa wananchi wengi kwa wakati mmoja". alisema.

Aidha, Wananchi wamehimizwa kuendelea kutumia elimu  ya sheria ili kuongeza uelewa wao kuhusu haki na wajibu wao, pamoja na kufuata taratibu zilizowekwa kisheria katika  ukamataji na haki za mtuhumiwa.