Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania hivi karibuni kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) mkoani Tanga, imetoa elimu kuhusu Sheria ya Michezo ya Kubahatisha, Sura 41 kwa wanafunzi na wadau mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria katika sekta hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mafunzo hayo mawakili wa Serikali kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ambao ni Vicky Mbunde, Baraka Chipamba na Latifa Mustapha walisema kuwa lengo kuu ni kuhakikisha vijana na jamii kwa ujumla wanapata uelewa sahihi kuhusu haki, wajibu na athari zinazohusiana na michezo ya kubahatisha kwa watoto.
Moja ya mawakili hao alibainisha kuwa kukosekana kwa elimu ya kutosha kumechangia baadhi ya wananchi na wamiliki wa michezo ya kubahatisha kuwahusha Watoto katika shughuli hizo bila kufahamu madhara yake ya kielimu, kisaikolojia, kijamii na kimaadili katika utawi wa watoto.
Awali akiwakaribisha Mawakili hao Makamu Mkuu wa chuo hicho Bw.Gideon Laurumbe alieleza kuwa mafunzo hayo yamekuja kwa wakati muafaka, hasa kwa vijana wanaojiandaa kuingia katika soko la ajira au kujiajiri, kwani yanawasaidia kufanya maamuzi sahihi na yenye tija.
Washiriki wa mafunzo hayo walipata fursa ya kujifunza kuhusu Sheria zinazosimamia aina mbalimbali ya michezo ya kubahatisha pamoja na wajibu walionao katika kulinda Watoto dhidi ya michezo hiyo.
Aidha, walihimizwa kuzingatia matumizi sahihi ya fedha na kuepuka utegemezi wa bahati nasibu kama chanzo kikuu cha kipato.
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki walieleza kufurahishwa na mafunzo hayo, wakisema yamewapa mwanga mpya kuhusu hatari zilizojificha katika michezo ya kubahatisha pamoja na umuhimu wa kufuata sheria.
Aidha wanafunzi hao waliomba serikali kuongeza usimamizi wa sheria ili kupunguza matangazo yasiyokuwa ya lazima kuhusu michezo hiyo pamoja na kuhakisha vifaa vinavyotumika katika michezo hiyo (Madubwi, Bonanza) vinawekwa sehemu maalumu kuliko hali ilivuo sasa ambapo vinapatikana hadharani katika maduka ya kawaida.
Tume ya Kurekebisha Sheria imeahidi kuendelea kutoa elimu kama hiyo katika maeneo mbalimbali nchini ili kujenga jamii yenye uelewa wa sheria na inayoweza kufanya maamuzi sahihi katika masuala ya kijamii na kiuchumi.