Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Tumesheria Bi. Angela Gombanila, amewahimiza watumishi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kujiunga na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya-Tawi la Tumesheria (TUGHE) ili kuimarisha sauti ya wafanyakazi na kulinda haki zao mahali pa kazi.
Gombanila ameeleza hayo leo wakati wa kikao na wajumbe wa kamati ya TUGHE tawi la Tumesheria huku akisisitiza kwamba chama hicho ni chombo muhimu kwa kila mtumishi wa Umma ndani ya Taasisi hiyo.
Aidha, amefafanua kwamba Mtumishi ana fursa ya kushiriki pamoja na wenzake katika kujadili na kutatua masuala yanayohusu utendaji kazi, stahili mahali pa kazi, haki mbalimbali, kujiandaa kustaafu na nidhamu eneo la kazi.
Bi. Gombanila aliendelea kueleza kwamba bila tawi kuwa na wanachama wa kutosha, chama hakitaweza kutekeleza majukumu yake kikamilifu hivyo kujiunga ni kuwekeza kwenye usalama wa mtumishi na maendeleo ya pamoja.
“Chama hakitaiishi bila wanachama; kila mmoja wetu anapojiunga, anachangia nguvu ya pamoja ambayo inatuletea tija kwa wote.”
Katika kikao hicho pia ilibainishwa kuwa tawi la TUGHE Tumesheria linahitaji kuongezeka kwa uandikishaji wa wanachama wapya ili kuweza kushughulikia vyema changamoto mbalimbali za kazi.
Hata hivyo Mwenyekiti alimalizia kwa kusema kwamba mpaka sasa chama kina idadi ndogo sana ya wanachama ikilinganishwa na idadi ya watumishi waliopo ambapo alieleza kwamba haitoshi kuwakilisha nguvu ya jumla ya wafanyakazi wote.
Kwa kuzingatia hilo, Mwenyekiti aliiomba Kamati za tawi kuandaa orodha ya watumishi, kutoa elimu na kuhamasisha ndani ya vitengo watumishi kujiunga kwa kusambaza fomu za usajili wa wanachama na kuwasajili.