Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania yatoa elimu ya Sheria kuhusu Makosa ya Kimtandao, Kwa wanafunzi wanaosoma chuo cha Ufundi Stadi VETA mkoani Mtwara ili kuwasaidia uelewa utakaowafanya waweze kuepuka Kutenda makosa hayo.
Elimu hiyo imetolewa tarehe 24 Aprili 2025 katika ukumbi wa chuo cha Ufundi VETA mkoani Mtwara ambapo zaidi ya wanafunzi 200 walishiriki katika kujifunza juu ya Sheria ya Makosa ya Kimtandao.
Akizungumza na wanafunzi hao Naibu katibu na Mkuu wa Kitengo cha elimu ya Sheria kwa Umma, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bi. Zainab Chanzi alibainisha kuwa Makosa ya kimtandao yamezidi kutokea kutokana na kukua kwa maendeleo ya Teknolojia na kubainisha kuwa ni Jinai inayojumuisha utendaji kosa kwa kutumia simu, kompyuta ama aina yeyote ya Teknolojia ya mawasiliano ambapo Naibu Katibu amewaasa wanafunzi hao kuwa makini wanapotumia vifaa vya mawasiliano kuepuka Kutenda makosa ya kimtandao.
“Hata inapotokea simu yako imepotea wahi katoe taarifa kituo cha polisi , usipofanya hivyo mwingine atakayeokota na akitenda uhalifu kwa kutumia simu hiyo yenye utambulisho wako maana yake wewe ndie utakaekamatwa” alisema Bi. Zainab
Akibainisha makosa hayo Afisa Sheria wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bi.Jackline Nungu, alieleza kuwa makosa ya Kimtandao yaliyoainishwa kwa mujibu wa Sheria ni Udukuzi,Ujasusi data, kughushi kwa kutumia kompyuta,Ulaghai kwa kutumia kompyuta,kuchapisha au kusambaza ponografia za watoto katika mitandao,kusambaza ponografia za watu wazima katika mitandao,kusambaza taarifa za uongo,kuharibu Ushahidi kwa kutumia simu au kompyuta wakati upelelezi ukiendelea, kudhalilisha watu kwa njia ya mtandao,wizi wa utambulisho wa mtu binafsi na kuchapisha maudhui ya kiubaguzi.
“Ni wajibu wenu kuepuka au kukataa kusambaza taarifa bila kuwa na uhakika, ikiwa kitu hauna uhakika nacho usikisambaze kwakua kufanya hivyo ni Kutenda kosa na ikithibitika unaweza kutiwa hatiani” alieleza Jackline.
Aidha Jackline aliendelea kueleza kuwa pamoja na majukumu mengine yanayotekelezwa na Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, lakini jukumu la kutoa Elimu ya Sheria kwa Umma linalenga kusaidia jamii kujiepusha na kujihusisha na vitendo vya uhalifu huku akitaja wazi mfano wa makosa ya kimtandao jinsi yanavyoweza kuleta madhara katika Uchumi wa Taifa, akitolea mfano wizi wa mtandaoni unavyoweza kuleta hasara za kiuchumi katika jamii .
Kwa upande wake Theresia Ibrahim ambae ni Mkuu wa Chuo cha VETA Mtwara ameishukuru Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kwa kufika chuoni hapo na kutoa elimu ya sheria na kueleza kuwa ni wakati muafaka kwa wanafunzi chuoni hapo kupatiwa elimu ya sheria kuhusu Makosa ya Kimtandao ambapo amesema elimu hiyo itakua msaada mkubwa wa kujilinda Kutenda makosa hayo kwani sehemu kubwa ya wanafunzi chuoni hapo ni watumiaji wa Simu Janja na wafuasi wa matumizi ya Mitandao ya kijamii.
“Tunawashukuru sana Tume kwa Elimu hii na tunawaomba wapange siku nyingine waje kutoa elimu ya sheria kwa muda wa kutosha zaidi, maana vijana wetu wana changamoto mbalimbali za kisheria hivi leo wamepata maarifa makubwa ya kujiepusha na makosa ya Kimtandao” alisema Theresia
Baadhi ya wanafunzi wakiwamo Bernadetha Benjamin na Frank Martin wamesema elimu ya sheria juu ya Makosa ya kimtandao hawakua wanafahamu na kwamba Tume imewapa mwanga wa kujilinda juu ya mkosa hayo na kuahidi kuwa mabaloz wazuri wa kuelimisha jamii juu ya sheria hiyo.
Tume ya Kurekebisha Sheria ipo mkoani Mtwara kwa lengo la kutoa elimu ya sheria kwa Umma kupitia mikutano ya wadau, semina mashuleni na vyuo vya kati ili kuisadia jamii kuwa na uelewa juu ya masulala ya kisheria.