Watu wenye mahitaji maalumu mkoani Mtwara wameishukuru Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kwa kuwajengea uwezo kuhusu Sheria ya Watu Wenye Ulemavu,Wosia na Mirathi, na Sheria ya Makosa ya Kimtandao ambapo waliungana na makundi mengine ya kijamii wakiwemo wanawake wajasiriamali, madereva bajaji na pikipiki,pamoja na viongozi wa dini ili kupata uelewa wa masuala ya kisheria.
Wakizungumza katika kikao cha wadau kilichofanyika tarehe 25/4/2025 katika ukumbi wa VETA mkoani Mtwara moja ya washiriki Bw. Athumani Chiwaula (58),mkazi wa Mtwara Mikindani alisema watu wenye ulemavu wamekua wakisahaulika kupata stahiki mbali mbali kutoka kwa jamii kutokana na kutojua sheria zinazobainisha haki na wajibu wao. Hivyo elimu waliyopata imewajengea uwezo na ujasiri katika kudai haki zao.
“Sheria inagawa haki ni ipi wajibu ni upi na lipi ufanye na lipi usilifanye, tunawashukuru sana hii Taasisi ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, kutupa nafasi watu wenye ulemavu kuchangia mawazo yetu” alisema Bw. Athumani.
Kwa upande wake Nasra Amani Khalid (27) ambae ni mratibu wa Chama Cha Watu Wasioona mkoani alisema amepata maarifa mapya juu ya masuala ya kisheria hususan taratibu za ufunguaji wa mashauri ya mirathi mahakamani na umuhimu wa kuandika wosia huku akikiri kuwa amewahi kutenda makosa ya kimtandao bila kutambua kuwa alikua akitenda makosa na kuahidi kuwa balozi wa kuelimisha wengine juu ya sheria hizo.
“Kuna makosa nimeyafanya kwenye mitandao lakini nilikua sijui kama makosa, haya mafunzo yamenisaidia sana na nipo tayari kutoa elimu kwa jamii nyingine” alisema Bi.Nasra.
Akizungumzia kuhusu utoaji wa elimu ya Sheria kwa makundi mbalimbali ya jamii Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya kurekebisha Sheria Bi. Zainab Chanzi alisema,kuwa na sheria nzuri na zikakaa katika vitabu tu bila kuzielewa haileti tija hivyo Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania inatoa elimu katika makundi tofauti ya jamii ili kuwajenga uwezo wadau mbalimbali kuhusu masula ya kisheria.
Bi. Zainab alisema malengo ya kutoa mada mbalimbali ikiwemo Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ni kujenga uelewa kwa jamii, kuhusu haki za makundi ya watu wenye mahitaji maalum ili sheria husika iwe na maana na iweze kutekelezwa ipasavyo.
“inapaswa watu wote wajue haki na wajibu wa watu wenye ulemavu na watu wengine ambao sheria imewapa majukumu ya kufanya ambayo yanaweza yakasaidia hizo haki kutekelezeka”. alisema Bi.Zainab
Aidha katika hatua hiyo pia Bi. Zainab alisema wamewajengea uwezo pia juu ya Sheria ya Makosa ya Kimtandao ili kukabiliana na ulimwengu wa kidigitali kwa kuwa maendeleo ya Sayansi na Teknolojia yanapaswa kuleta matokeo chanya katika jamii na si kudhoofisha