Katibu mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Bw. George Mandepo, amesema ushiriki wa Tume hiyo katika maonesho ya 49 ya kimataifa ya biashara ni kwa lengo la kutoa elimu ya sheria kwa Umma juu ya sheria mbalimbali pamoja na kutoa ushauri wa kisheria kwa wananchi na kupokea maoni ya wananchi ya mapendekezo au maboresho ya sheria mbalimbali za Tanzania.
Mandepo aliyasema hayo Julai 7,2025 akiwa katika banda la Tume hiyo katika viwanja vya maonesho ya Sabasaba Jijini Dar es salaam na kueleza kuwa mchakato wa upokeaji wa maoni kutoka kwa wananchi husaidia tume hiyo kuanzisha mchakato wa kutunga au kurekebisha sheria ambapo alisema katika maonesho ya Sabasaba hupokea watu wengi ambao wanapata nafasi ya kutoa maoni yao pamoja na kupata elimu na ushauri wa kisheria juu ya sheria mbalimbali.
“Tupo hapa katika viwanja vya Sabasaba kwa ajili ya kutoa elimu ya sheria kwa Umma, lakini pia kupokea maoni ya Wananchi kwa sababu sheria ni maisha na maisha ni sheria, hakuna mtu naweza kuishi bila sheria” alisema Mandepo.
Katika hatua hiyo pia Mandepo alieleza kuhusu Tume hiyo kuanza mchakato wa kufanya utafiti kuhusu mifumo ya sheria inayosimamia michezo ya kubahatisha, Uvutaji wa tumbaku pamoja na vilevi nah ii ni kutokana na kukithiri kwa vitendo visivyo na maadili hasa kwa vijana.
Alisema tafiti hizo zimeanza ili kuishauri serikali na kuon ameneo gani yanapaswa kurekebishwa kutokana na kuongezeka kwa idadi kubwa ya vijana nchinihasa Watoto wa kike kujiingiza zaidi katika uvutaji wa wa Shisha.
Kwa upande wake Naibu katibu wa Tume hiyo ambae ni mkuu wa kitengo cha elimu ya sheria kwa Umma Bi. Zainab Chanzi alisema uelewa kwa Wananchi kuhusu sheria mbalimbali nchini bado si wa kutosha hivyo hatua ya Tume hiyo kuendelea kutoa elimu kwa njia mbali mbali ikiwamo vipindi vya redio na televisheni pamoja na kushiriki maonesho mbalimbali ikiwamo Sabasaba lengo ni kuisaida jamii kua na uelewa toshelezi kuhusu masuala ya kisheria ili waweze kuishi kwa utii wa sheria bila shuruti.
“Uelewa wa sheria kwa wananchi bado haupo katika kiwango cha juu sana lakini tunajitahidi kadri tunavyoweza, tunafanya makongamano, tunafanya vipindi vya redio na hata kushiriki maonesho kama haya ya Sabasaba ili kuendelea kutoa elimu ya sheria kwa wananchi”. Alisema Zainab
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ni Miongoni mwa Taasisi zinazoshiriki katika Maonesho ya 49 ya kimataifa ya biashara yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba Jijini Dar es salaam kwa lengo la kutoa Ushauri wa kisheria kutoa elimu ya sheria kwa Umma pamoja na kupokea maoni ya wananchi juu ya mapendekezo ya maboresho ya Sheria mbalimbali nchini.