Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

TUME YA KUREKEBISHA SHERIA YAPANGA MIKAKATI YA KUTEKELEZA DIRA YA TAIFA 2050
08 Aug 2025
TUME YA KUREKEBISHA...




Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) leo tarehe 7 Agosti, 2025 imeeleza namna ilivyojipanga kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kwa kufanya maboresho katika mifumo ya sheria ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya vizazi vijavyo na kuendana na mabadiliko ya teknolojia, jamii na mazingira duniani.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Naibu Katibu wa Tume hiyo, Bi. Zainab Chanzi, alisema kuwa Dira ya Taifa ya 2050 ni dira pana na ya kipekee inayolenga kuiwezesha Tanzania kuwa Taifa jumuishi lenye ustawi, haki na linalojitegemea.

“Ili Dira ya 2050 iweze kufikiwa, sheria ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa Dira, hivyo sheria zetu lazima ziakisi misingi, nguzo na shabaha za Dira hiyo. Kama Tume, tumejipanga kuhakikisha sheria zinafanyiwa mapitio, tafiti na tathmini na wananchi kuelimishwa maboresho ya sheria kwa lengo la kujenga uelewa kwa wananchi,” alisema Bi. Chanzi.

Aidha Bi. Chanzi alibainisha mikakati mbalimbali ambayo Tume imepanga kutekeleza imiwemo kupitia Sheria zilizopitwa na wakati ili kuhakikisha hazikwamishi maendeleo ya kisasa kama vile matumizi ya akili unde (AI).

Akizungumzia kuhusu sekta ya Kilimo Bi. Zainab alieleza umuhimu wa Sekta ya Kilimo kwa kuwa kwa mujibu wa Dira 2050 ni miongoni wa sekta ya mageuzi hivyo kama Tume imejipanga kuhakikisha sheria zinazosimamia sekta hii zinaakisi matarajio yaliyowekwa na Dira kama vile kuwa Taifa linaloongoza katika uzalishaji wa chakula.


“Sheria tunazotunga leo ndizo zitakazojenga Tanzania ya baadaye. Hivyo basi, kazi yetu ni kuhakikisha msingi huo wa kisheria unawekwa kwa weledi, umakini na mshikamano wa kitaifa,” aliongeza.