Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) imeendelea kutoa elimu ya sheria kwa wananchi wanaoshiriki katika Maonesho ya Wakulima ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma ambapo elimu juu ya Sheria ya Ustawi wa Wanyama, Sura Na. 154, ilitolewa kwa makundi mbalimbali ya wafugaji kutoka mikoa tofauti ya Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kukutana na wafugaji hao Agosti 4, 2025 katika Viwanja vya Nanenane Nzuguni mkoani Dodoma, Wakili wa serikali kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Vick Mbunde amesema kuwa lengo kuu la elimu hiyo ni kuwawezesha wafugaji kufahamu haki za wanyama wanaowafuga na wajibu wao katika kuwahudumia wanyama hao, kama sheria inavyoainisha.
“Wafugaji wengi hawafahamu uwepo wa sheria inayowataka kuwahudumia vyema wanyama wao, ikiwemo kuhakikisha wanapata chakula cha kutosha, maji safi, malazi bora, na matibabu. Sheria ya Ustawi wa Wanyama inalinda maslahi ya wanyama dhidi ya mateso, manyanyaso na mazingira duni ya maisha,” alisema Vick.
“Sheria ya Ustawi wa Wanyama, Sura Na. 154, inalenga kuhakikisha kuwa wanyama wote wanaofugwa au kutunzwa na binadamu wanapokea huduma stahiki, na Sheria inatoa adhabu kwa yeyote anayekiuka masharti ya sheria hiyo”. Aliongeza kueeleza
Katika maonesho hayo, Tume pia imekuwa ikigawa vipeperushi vyenye maelezo ya msingi kuhusu Sheria hiyo pamoja na kutoa nafasi kwa wananchi kuuliza maswali na kupata majibu ya kitaalamu kuhusu masuala ya kisheria yanayohusu mifugo na wanyama kwa ujumla.
Hosea Godwin ambaye ni Mfugaji anasema ameipongeza Tume hiyo kwa jitihada hizo na kwamba elimu iliyotolewa imewasaidia kufahamu masuala ambayo hapo awali hawakuyatilia maanani.
“Nilikuwa sifahamu kuwa ukimtesa mnyama, kama kumpiga hovyo au kumwacha bila chakula kwa siku kadhaa, ni kosa na unaweza kuchukuliwa hatua za kisheria. Hii ni elimu muhimu sana kwetu sisi wafugaji,” alisema Hosea
Tume ya Kurekebisha Sheria inatarajia kuendelea na kampeni zake za kutoa elimu ya sheria katika maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kujenga jamii inayozingatia sheria na haki za kila kiumbe hai.
Mwisho