Timu za Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (Tume Sheria Sport Club) Wanaume na Wanawake zimeibuka na ushindi katika mashindano kuvuta kamba michuano ya SHIMIWI inayoendelea Jijini Mwanza.
Michuano hiyo iliyoanza leo tarehe 1/9/2025 katika uwanja wa Furahisha, Timu ya kuvuta kamba ya Wanawake wa Tumesheria walipata ushindi kwa kuwavuta Timu ya Uwekezaji ambao wote wamepangwa kundi E katika mashindano hayo ya uvutaji wa kamba.
Timu ya Wanaume Tumesheria nao walipata Ushindi dhidi ya Timu ya Bunge wote wakiwa kundi D ambapo Bunge hawakutokea uwanjani na kwa mujibu wa taratibu kuwa timu isiyofika ushindi wanapewa timu iliyofika ndipo Tume wakajinyakulia ushindi huo wa bure kwa mpinzani kutotokea eneo la mashindano.
Hatua hii ni mzunguko wa kwanza wa makundi katika mashindano ya kuvuta kamba huku mzunguko wa pili ukitegemewa kuendelea hapo kesho tarehe 2/9/2025 na kwa mujibu wa ratiba Timu ya Wanaume Tumesheria watashindana kuvuta kamba na Timu ya W/Sera huku Timu ya wanawake wakitegemea kuingia mchezoni tarehe 3/9/2025 kuchuana na Timu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote UCSAF.
Michuano ya SHIMIWI imeanza rasmi Septemba mosi mwaka huu na kutegemewa kuhitimishwa tarehe 16 Septemba 2025 huku zaidi ya timu 70 zikitegemewa kushiriki michezo mbalimbali ikiwamo kuvuta kamba, Mpira wa pete, mpira wa miguu, bao, drafti, riadha na mingineyo.