Government Logo
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano,Atembelea Banda la LRCT.
04 Aug 2025
Naibu Katibu Mkuu Of...

Naibu Katibu Mkuu  Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano, Bw. Abdala Mitawi, leo tarehe 3.07.2025 ametembelea banda la Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (LRCT) katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, ambako Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanaendelea.

Katika ziara hiyo, Bw. Mitawi alipokelewa na maafisa wa Tume  ambao walimpa maelezo ya kina kuhusu majukumu ya Tume hiyo, mafanikio yaliyopatikana hadi sasa, na nafasi ya Tume katika kuboresha mazingira ya kisheria nchini .

Bw. Mitawi alionesha kufurahishwa na kazi inayofanywa na Tume hiyo, hususan jitihada zake za kupitia, kupendekeza, na kuandaa marekebisho ya sheria mbalimbali ili ziendane na wakati, na kutatua changamoto za kiutendaji, kijamii na kiuchumi.

“Nimeridhishwa na kazi mnayoifanya, hususan katika kuhakikisha kuwa sheria zinazotumika nchini zinaendana na mabadiliko ya kijamii na kiteknolojia, alisema Bw. Mitawi.

Akiwa katika banda hilo, Naibu Katibu Mkuu alipata fursa ya kuangalia machapisho mbalimbali ya kisheria yaliyoandaliwa na Tume, pamoja na kupokea maelezo kuhusu mchakato wa ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wananchi kabla ya sheria kurekebishwa.

Tume ya Kurekebisha Sheria ni chombo huru cha Serikali kinachowajibika kwa kuishauri Serikali juu ya mapendekezonya marekebisho ya sheria ili kuhakikisha zinabaki kuwa sahihi, zenye uwiano, na zinazotekelezeka kwa ufanisi.

Maonesho ya Nanenane mwaka huu yanafanyika kuanzia Agosti 1 hadi 8, yakihusisha taasisi mbalimbali za Serikali, binafsi, na asasi za kiraia, zikiwemo zile zinazojihusisha na sheria, kilimo, elimu, afya, na teknolojia ambapo Tume ya kurekebisha Sheria inashriki katika maonesho hayo ili kutoa elimu ya sheria kwa Umma, kupokea maoni ya mapendekezo ya Sheria na kutoa ushauri wa kisheria.